
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi.
Na Mwandishi Wetu
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mabadiliko ya ratiba ya mchakato wake wa ndani wa kuwateua wagombea wa nafasi za ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2025.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho tawala, Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi jijini Dodoma juzi, inaeleza kuwa mabadiliko hayo ya ratiba yanafuatia mashauriano yaliyofanyika na wana-CCM, tafakuri na kupima ushauri uliotolewa kwa maslahi ya chama kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Kwa kuzingatia marekebisho yaliyofanyika, sasa mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani utaanza Juni 28 na kukamilika Julai 2, 2025.
Aprili 10, 2025, CCM ilitangaza kwamba shuhuli hizo zingefanyika kati ya Mei 1 na 15, 2025.
Utaratibu unaelekeza kwamba wagombea wa nafasi hizo za uongozi wanatakiwa kuchukua na kurudisha fomu za uteuzi kutoka kwa katibu wa CCM wa wilaya husika.
Kwa mujibu wa taarifa, wagombea wa Viti Maalum vya Wanawake katika Bunge na Baraza la Wawakilishi kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na makundi maalum watachukua fomu na kuzirudisha kwa Katibu wa UWT wa Mkoa husika.
Wagombea wa Viti Maalum vya Wanawake kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) katika Bunge na Baraza la Wawakilishi watachukua fomu na kuzirudisha kwa Katibu wa UVCCM mkoa husika.
Kwa wagombea wa Viti Maalum vya Wanawake katika Bunge na Baraza la Wawakilishi kupitia Jumuiya ya Wazazi, taarifa imeeleza kuwa watachukua fomu na kuzirudisha kwa Katibu wa Wazazi mkoa husika.
Wagombea wa nafasi za udiwani wa Kata au Wadi kwa upande wa Tanzania Visiwani, wao watachukua fomu na kuzirudisha kwa Katibu wa CCM wa Kata au Wadi inayohusika.
Nao wagombea wa udiwani Viti Maalum vya Wanawake watachukua fomu zao na kuzirudisha kwa Katibu wa UWT wa wilaya husika.
No comments:
Post a Comment