NEWS

Wednesday, 7 May 2025

Grace Entertainment and Promotion kufanya tamasha kubwa la utamaduni Mara



Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Grace Entertainment & Promotion, Grace Revocatus Shija, akizungumza na Mara Online News mjini Tarime leo Mei 7, 2025.
---------------------------------------

Na Joseph Maunya, Tarime

Kampuni ya Grace Entertainment & Promotion imepanga kufanya tamasha kubwa la utamaduni mkoani Mara linalojulikana kama "Mara Intercultural Festival 2025", litakalohusisha mashindano ya vikundi vya michezo ya asili kutoka makabila mbalimbali ya mkoani hapa.

Akizungumza na Mara Online News mjini Tarime leo Jumatano, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Grace Revocatus Shija, amesema moja ya malengo makuu ya tamasha hilo ni kuhamasisha maendeleo, hasa uwekezaji katika mkoa wa Mara ambao umejaaliwa kuwa na fursa lukuki za kiuchumi.

"Dhima ya tamasha hilo ni kuhamasisha wazawa wa mkoa wa Mara walio nje ya mkoa kurudi kuwekeza mkoani kwetu na kuendeleza utalii wa kiutamaduni.

"Hivyo, tunaandaa tamasha kubwa la Mara Intercultural Festival kwa lengo la kuvishindanisha na kuvipa heshima vikundi vyetu vya ngoma za asili kutoka makabila mbalimbali mkoani Mara, pamoja na kutangaza fursa zilizopo kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na nje ya mkoa.

"Pia, kutakuwa na zawadi kwa vikundi vitakavyoshinda pamoja na zawadi kwa vikundi vyote vitakavyotenga muda wao kuja kushiriki nasi katika tamasha hili kubwa la kiutamaduni," amesema Grace.

Ameweka wazi kuwa uzinduzi wa tamasha hilo utafanyika Mei 23, 2025 katika uwanja wa Obwere uliopo Shirati wilayani Rorya.

Tamasha hilo pia litaendelea katika maeneo mengine ya mkoa wa Mara ambapo Musoma litafanyika Mei 30, Serengeti Juni 7, Nyamongo Juni 14 na kilele cha tamasha hilo litafanyika Julai 4 na 5, 2025 mjini Tarime kwenye uwanja wa Serengeti “Shamba la Bibi”.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages