NEWS

Thursday, 8 May 2025

Rais Samia atangaza siku saba za maombolezo kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya



Mzee Cleopa David Msuya enzi za uhai

Na Mwandishi Wetu

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amelitangazia taifa kifo cha Mzee Cleopa David Msuya, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kilichotokea jana Mei 7, 2025 saa tatu asubuhi katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam.

Mzee Msuya alikuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo katika hospitali hiyo.

“Hayati Cleopa David Msuya ameugua kwa muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu ndani na nje ya nchi, ikiwemo katika Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Mzena na kule jijini London [nchini Uingereza],’’ Rais Samia alisema jana wakati akitangaza kifo hicho.

Rais Samia pia alitangaza siku saba za maombolezo ya msiba huo kuanzia jana Mei 7 hadi 13, 2025 ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti nchini.

Aidha, Rais Samia alituma salamu zake za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huo.

“Taarifa zaidi kuhusu msiba huu zitaendelea kutolewa na serikali, poleni sana Watanzania,” Rais Samia alisema kwa masikitiko.

Cleopa David Msuya alizaliwa Januari 4,1931 huko Chomvu Usangi, Wilaya ya Mwanga, mkoaNI Kilimanjaro ambapo alisoma Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda kati ya mwaka 1952 na 1955 na kisha kufanya kazi za maendeleo vijijini hadi mwaka 1964.

Kuanzia mwaka huo, Msuya alihudumu kama Katibu Mkuu katika wizara mbalimbali hadi mwaka 1972, alipoteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na baadaye kushika nyadhifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Waziri wa Viwanda, Waziri Mkuu (1980–1983 na tena 1994–1995), na Waziri wa Fedha na Mipango hadi mwaka 1994.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Msuya alibaki kuwa Mbunge wa Jimbo la Mwanga hadi alipostaafu mwaka 2000.

Hata baada ya kustaafu, aliendelea kushiriki katika siasa kupitia chama tawala - CCM na alikuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo la Kilimanjaro.

Oktoba 23, 2019, Msuya aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Ardhi akiwa na umri wa miaka 88.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages