
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi (katikati), akipata maelezo kutoka kwenye banda la Mji Mkongwe Bagamoyo na Kaole wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Urithi wa Dunia, Afrika 2025 yaliyofanyika kitaifa mjini Mugumu, Serengeti jana. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kemirembe Lwota.
-----------------------------------
Na Christopher Gamaina, Serengeti
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, ametoa wito kwa taasisi za uhifadhi kuongeza jitihada katika kuelimisha jamii na kuimarisha ulinzi wa maeneo ya urithi wa dunia nchini, akisisitiza umuhimu wa kuyahifadhi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Kanali Mtambi aliyasema hayo katika Maadhamisho ya Siku ya Urithi wa Dunia kwa Afrika 2025 yaliyofanyika kitaifa wilayani Serengeti jana Jumatatu, Hifadhi ya Taifa Serengeti ikiwa mwenyeji wa tukio hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, akihutubia katika maadhimisho hayo.
-----------------------------------
“Katika bara la Afrika kuna maeneo ya urithi wa dunia 147, kati ya hayo, saba yapo Tanzania na yameifanya nchi yetu kuwa kivutio kukubwa cha utalii, hivyo yanastahili kuimarishiwa ulinzi ili yawe endelevu,” alisema Kanali Mtambi huku akiwataka watu kutojihusisha na uharibifu wa maeneo hayo.
Alisisitiza pia umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika kuelimisha jamii iweze kuyafahamu maeneo hayo na faida zake kwa taifa na dunia.
Sambamba na hilo, Kanali Mtambi alizishauri taasisi za uhifadhi kama vile Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlala ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuimarisha uhusiano na jamii inayozunguka maeneo hayo ili iweze kutoa ushirikiano wa dhati katika kuyalinda.
Aidha, aliwapongeza wananchi mbalimbali waliojitokeza kushiriki katika maadhimisho hayo na kupata elimu na hamasa ya kulinda maeneo ya urithi wa dunia.
Awali, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Stephano Msumi, alitoa wito kwa jamii na wadau mbalimbali kuwa tayari kusaidia kuimarisha ulinzi wa maeneo hayo yenye sifa za kipekee kitaifa na kimataifa.
Maeneo ya urithi wa dunia yaliyopo Tanzania ni Hifadhi ya Taifa Serengeti, Hifadhi ya Taifa Mlima Kilimanjaro, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Pori la Akiba la Selous, Mji Mkongwe wa Zanzibar, Michoro ya Miambani ya Kondoa na Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.
Maeneo hayo yalitangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (United Nations Educational, Scientific and Cultural Organisation - UNESCO) kuingizwa kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia.

Kikosi cha Bendi (Brass Band) ya TANAPA kikiongoza maandamano ya washiriki wa maadhimisho hayo.
-------------------------------------
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Urithi wa Dunia, Afrika 2025 inasema: “Majanga na Migogoro ni Tishio kwa Maeneo ya Urithi wa Dunia”.
Maadhimisho hayo ambayo yalianza kwa matembezi ya washiriki ya kilomita tatu, yalihudhuriwa pia na shirika la kimataifa la uhifadhi la Frankfurt Zoological Society (FZS) – Serengeti na Nyansaho Foundation.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
»Ajali yakatisha maisha ya Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji Tarime
»Mara: Hoteli ya kifahari ya CMG yazinduliwa kwa kishindo Tarime
»Waziri Mavunde azindua mradi wa uchimbaji madini kwa vijana Nyamongo
»MAKALA:Ushirika wa WAMACU wamshukuru Rais Samia uzinduzi wa Benki ya Ushirika Tanzania
No comments:
Post a Comment