
Na Mwandishi Wetu
Huduma mbalimbali kwenye sekta ya madini ambazo zilikuwa zikitolewa maeneo tofauti, sasa zimehamishiwa wizarani kufuatia kukamilika kwa jengo la makao makuu ya wizara husika eneo la Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, aliuambia mkutano uliohudhuriwa na viongozi wa menejimenti ya wizara, taasisi na wafanyakazi jana kuwa uhamisho wa huduma hizo unatokana na kukamilika kwa ujenzi wa jengo la wizara yake.
Mavunde alisema upatikanaji wa huduma eneo moja utaondoa usumbufu kwa wadau wa wizara ambao walikuwa wakilazimika kwenda eneo moja hadi jingine kutafuta huduma hizo.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, aliishukuru serikali kwa kuwezesha ujenzi wa jengo la makao makuu ya wizara ambalo litakuwa na miundombinu inayohitajika kwa tasnia ya madini.
March 25, mwaka huu, Waziri Mavunde aliiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwamba shughuli zote za wizara zitahamishiwa Dodoma baada ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo la wizara.
Jengo hilo lililogharimu shilingi bilioni 22.8 limejengwa na Shirika la Nyumba la Taifa chini ya ushauri wa Wakala wa Majengo Tanzania.
No comments:
Post a Comment