NEWS

Sunday, 18 May 2025

Watoa huduma migodini tumieni utulivu uliopo kuchangamkia fursa mbalimbali - TAMISA




NA MWANDISHI WETU, Dar

CHAMA Cha Watoa Huduma Sekta ya Madini (TAMISA) kimetakiwa kutumia hali ya amani na utulivu iliyopo kwenye tasnia hiyo kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo ili kupata mafanikio.

Pia, kimetakiwa kujipanga na kuwadhibiti wanachama wake wasio waaminifu katika utoaji wa huduma.

Ushauri huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahya Samamba, wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Masoko na Mawasiliano ya chama hicho, ambapo alisititiza kwamba kuwepo kwa amani na utulivu kwenye sekta ya madini ni nguzo ya mafanikio.

Akizizungumzia uaminifu, Samamba alisema sekta ya madini inahitaji mtaji mkubwa na hivyo mtu anapowekeza fedha zake anaamini ziko katika mikono salama chini ya watu waadilifu.

Aliitaka TAMISA kuwa na meno ya kungáta kama ilivyo Bodi ya Usajili Wahandisi inavyowashughulikia wanachama wake wanaoharibu kazi, lengo likiwa ni utoaji wa huduma bora kwenye tasnia inayohusika.

Kamishna wa Tume ya Madini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji Watanzania katika Sekta ya Madini, Dkt. Theresia Numbi, alisema mabadiliko ya Sheria ya Madini inaweka usimamizi thabiti katika utekelezaji wa masuala ya ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini.

Dkt. Numbi alisema utekelezaji na ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini umeibua na kuchochea uongezekaji wa fursa mbalimbali katika nafasi za ajira na mafunzo, uhaulishaji wa teknolojia, utafiti na maendeleo pamoja na matumizi ya huduma na bidhaa zinazotolewa na kuzalishwa na Watanzania.

“Suala hili limeigeuza sekta ya madini kuwa na mchango mkubwa kuboresha maisha ya Watanzania na kuwapa fursa ya kukua kiuchumi na kiteknolojia,” alisema Dkt. Numbi.

Alisema Wizara na Tume ya Madini vitaendeleza usimamizi wa ushirikishwaji Watanzania na kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa huduma na bidhaa zinazotolewa na kuzalishwa nchini ili kuwanufaisha wazawa.

Naye Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Biashara ya Madini wa Tume ya Madini, Venance Kasiki, alisema “ni wakati sahihi kwa wazawa kushirikiana pamoja na TAMISA kuchangamkia fursa” zilizopo kwenye tasnia ya madini.

Mwenyekiti wa TAMISA, Peter Kumalilwa, alisema matarajio ya chama hicho ni kuona kwamba shilingi trilioni 3.1 zinazotajwa kama fursa kwa wazawa watoa huduma migodini zinaakisiwa moja kwa moja na Watanzania wote na kwamba kupitia TAMISA wanachama wake watanufaika.

Naye Mwenyekti wa Kamati iliyozinduliwa ya Masoko na Mawasiliano, Dkt. Sebastian Ndege, alisema huu ni wakati muafaka kwa Watanzania kushiriki katika uchumi wa madini kwa sababu nchi yao imejaaliwa kuwa na kila aina ya raslimali hiyo.

“Sisi kama TAMISA kazi yetu kubwa itakuwa kuwasimamia wanachama wetu kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na weledi na kwamba tunafuata maadili katika utoaji huduma,” alisema Dkt. Ndege.

TAMISA ilianzishwa Septemba 16, 2024 ili kusimamia watoa huduma katika sekta ya madini ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages