NEWS

Saturday, 24 May 2025

Mara Press Club walivyoadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, DC Meja Gowele awapongeza



Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (katikati waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mara Press Club, waandishi wa habari na wadau mbalimbali wa maendeleo waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari mkoani Mara jana Mei 23, 2025.
-----------------------------------------

Na Christopher Gamaina, Tarime

Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (Mara Regional Press Club – MRPC) imeadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mafanikio makubwa huku ikiungwa mkono na serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo

Maadhimisho hayo yalifanyika katika Hoteli ya CMG mjini Tarime jana Mei 23, 2025, mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Flowin Gowel, ambaye aliipongeza klabu hiyo kwa hatua hiyo.
Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia mada ukumbini katika maadhimisho hayo.
-------------------------------------

Aidha, katika hotuba yake, Meja Gowele alieleza kufurahishwa na namna MRPC inavyoendelea kuwaunganisha waandishi wa habari, sambamba na kujenga uhusiano na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani Mara.

Pia, aliwapongeza wanahabari hao kwa kuendelea kuisaidia serikali kutangaza mambo mazuri, zikiwemo fursa za maendeleo zilizopo mkoani Mara. “Mazuri yanayofanyika Mara ninyi [waandishi wa habari] ndio mnayafikisha kwa jamii,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mejea Edward Gowele (katikati), Mwenyekiti wa MRPC, Jacob Mugini (kushoto) na Katibu Mtendaji wa klabu hiyo, Pendo Mwakyembe, wakifurahia jambo wakati wa maadhimisho hayo.
-----------------------------------------

Meja Gowele alitumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha wanahabari kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo, kusimamia ukweli, kuwa na uzalendo na kutanguliza maslahi ya taifa katika kazi zao.

“Naomba tuandike habari zenye maslahi ya taifa, kalamu na habari zenu zisaidie pia kupata viongozi bora katika jamii,” aliongeza Meja Gowele.

Hata hivyo, alitoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari vya kidijitali ambavyo bado havijasajiliwa, kuhakikisha wanavisajili ili kuviendesha kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele (katikati), akimkabidhi mwaandishi wa habari Ghati Msamba cheti kilichotolewa na MRPC kumpongeza kwa mchango wake wa maendeleo ya klabu hiyo.
---------------------------------------

Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele (katikati), akimkabidhi Mwenyekiti wa MRPC, Jacob Mugini, zawadi iliyotolewa na waandishi wa habari kutambua kazi nzuri anayofanya kwa maendeleo ya klabu hiyo na wanachama wake.
--------------------------------------------

Mapema kabla ya hotuba ya mgeni rasmi, Mwenyekiti wa MRPC, Jacob Mugini, alisema mafanikio ya maadhimisho hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya klabu hiyo, waandishi wa habari, serikali na wadau wa maendeleo mkoani Mara.

Mugini alibainisha pia kuwa MRPC iko mbioni kuzindua mradi maalum wa kuwajengea waandishi wa habari wa mkoani Mara uwezo wa kuongeza ubora na ufanisi wa kazi zao, ili pia waweze kushiriki mashindano ya tuzo za uandishi mahiri za kitaifa na kimataifa.

Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele (katikati waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa MRPC na wadau wa maendeleo walioshiriki maadhimisho hayo.
---------------------------------------

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani mwaka huu wa 2025 ni: “Uhabarishaji katika Dunia Mpya: Mchango wa Akili Mnemba kwenye Uhuru wa Vyombo vya Habari,”

Maadhimisho hayo ya mkoani Mara yalipata udhamini kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo, wakiwemo Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Stanley Engineering Co. (T) Ltd, PKM Ltd, Waracha Company Ltd, MamaLeah Hardware, NBA, Chichake, Professor Mwera Foundation, Kemanyanki Group, MUWASA, CMG Hotel, Mara Online na Matiko Foundation, miongoni mwa wengine.

Mwaandishi wa habari Dinna Maningo (kushoto) akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya Akili Mnemba (AI) katika maadhimisho hayo.
-------------------------------------------
--------------------------------------------
Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele (katikati), akikabidhi zawadi kwa mwandishi wa habari Fresha Amos aliyewasilisha mada kuhusu umuhimu wa usalama wa kidijitali katika uandishi wa habari.
-----------------------------------------------
Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele (katikati), akikabidhi zawadi kwa mwandishi wa habari Helena Magabe aliyewasilisha mada kuhusu uandishi wa habari za uchaguzi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages