NEWS

Monday, 19 May 2025

Ofisi ya CAG yaendesha mafunzo kwa asasi za kiraia Mara



Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Nje Mkoa wa Mara, John Manoti Elius, akiwasilisha taarifa ya ofisi ya CAG katika mafunzo maalum kwa asasi za kiraia mjini Musoma, Mara wiki iliyopita. (Picha na Mara Online News)
-------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Musoma

Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (GAG) imeendesha mafunzo maalum kwa asasi za kiraia za mkoani Mara kuhusu ukaguzi wa hesabu za serikali unavyofanyika maeneo mbalimbali, ikiwemo ngazi ya serikali za mitaa na namna wanavyoweza kushirikiana na ofisi hiyo kwa maslahi ya jamii kwa ujumla.

Mafunzo hayo yalifanyika mjini Musoma wiki iliyopita kwa lengo la kuwezesha wadau mbalimbali kuelewa vizuri majukumu ya ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, dhima ya ripoti ya ukaguzi na namna wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya CAG.

"Tumekuja kuelekeza kazi moja ya kushirikiana na wadau wetu ambao ni asasi za kiraia kwa idhini ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Charles Kichere, kwa madhumuni ya kusambaza elimu ya ukaguzi kwa asasi za kiraia," alisema Mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Focus Mauki.

Aliongeza: "Kingine cha muhimu, tumekutana na asasi za kiraia kwa sababu ni mpango mkakati wetu wa ofisi ya ukaguzi unaotutaka kufanya mashirikiano na wadau mbalimbali, wakiwemo wakaguliwa, Bunge, waandishi, vyombo vya utekelezaji wa sheria kama mahakama, Jeshi la Polisi, TAKUKURU na asasi za kiraia."
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT), Rhobi Samwelly, alishukuru kupata fursa hiyo akisema mafunzo hayo yatakuwa na manufaa kwa walengwa.

"Mafunzo haya nayaona ni mazuri sana, yatatusaidia kuona kwamba rasilimali zinazotolewa zinafanya kazi kwa usahihi na kwa eneo sahihi," alisema Rhobi na kuongeza:

"Nipende kutoa wito kwa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kupokea mafunzo haya ili tuweze kusaidia kutoa taarifa kwa CAG, sisi wote ni wadau wa maendeleo."

Rhobi Samwelly akizungumza 
katika mafunzo hayo.
---------------------------------

Awali, Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Nje Mkoa wa Mara, John Manoti Elius, akisoma taarifa ya ofisi ya CAG, alisema: "Mafunzo haya yanatufungulia ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, na asasi za kiraia zitakuwa mabalozi wazuri wa kusambaza taarifa za ukaguzi kwa jamii kusaidia kuongeza elimu na uelewa wa kazi za ukaguzi kwa wananchi."
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages