NEWS

Wednesday, 21 May 2025

Tanzania, Namibia kuongeza juhudi za kukuza ushirikiano wa kiuchumi



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (kulia), akiwa na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Namibia, Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, mara baada ya kuwasili Ikulu, jijini Dar es Salaam jana Mei 20, 2025.
---------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Namibia zimekubaliana kuongeza juhudi za kukuza ushirikiano wa kiuchumi kwa kutafuta njia madhubuti za kukuza biashara baina yao, ikiwa ni pamoja na kuwezesha uwepo wa miradi mikubwa ya uwekezaji kutoka pande zote mbili.

Wakizungumza na vyombo vya habari, yeye na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Namibia, Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, mara baada ya mazungumzo rasmi, Rais Dkt. Samia alisisitiza umuhimu wa sekta binafsi katika kuchochea ajira kwa vijana na kupunguza umasikini.

Aidha, Marais hao walieleza dhamira ya kupanua ushirikiano katika maeneo ya elimu, utalii, mazingira, mifugo, uvuvi na nishati na kuweka msisitizo kwa sekta binafsi kuwekeza kwa kiwango kikubwa, tofauti na hali ilivyo sasa.

Rais Dkt. Samia alibainisha kuwa biashara kati ya Tanzania na Namibia imeongezeka kutoka shilingi bilioni 17 hadi bilioni 20 kati ya mwaka 2019 na 2023; ingawa hata hivyo, alisema kiwango hicho bado ni kidogo kulinganisha na fursa zilizopo na hivyo kuwataka wafanyabiashara wa nchi hizo mbili kuchangamkia fursa hizo.

Vilevile, Rais Dkt. Samia aliikaribisha sekta binafsi ya Namibia kuja kuwekeza na kushirikiana na Tanzania katika sekta za uongezaji thamani wa mifugo, uvuvi na katika sekta ya utalii.

Kuhusu utamaduni, Rais Dkt. Samia alisema Tanzania na Namibia zinatarajia kushirikiana katika sesta ya elimu, ambapo Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kitashirikiana na Chuo cha Triumphant cha Namibia kufundisha lugha ya Kiswahili kama njia ya kukuza uhusiano, urafiki na mshikamano wa kijamii.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages