NEWS

Monday, 9 June 2025

Uhifadhi wa mazingira: Barrick North Mara kupanda miti 50,000 kulinda mto Tighite



Viongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, vijiji, kata na Jumuiya ya Watumia Maji wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupanda miti ya asili kandokando ya mto Mara kijijini Matongo, Tarime wiki iliyopita.
--------------------------------------------

Na Christopher Gamaina

Asubuhi ya Juni 5, 2025, historia mpya iliandikwa katika kijiji cha Matongo, wilayani Tarime - pale viongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Jumuiya ya Watumia Maji na vijiji jirani walipokutana kutekeleza tukio la kupanda miti ya asili kandokando ya mto Tighite.

Walichukua muda wa takriban saa moja kukamilisha shughuli hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu wa 2025, ambapo kwa upande wa Tanzania kaulimbiu ya maadhimisho hayo inasema "Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo – Tuwajibike Sasa; Dhibiti Matumizi ya Plastiki".

Dhumuni la kupanda miti hiyo ni kuzuia mmomonyoko wa udongo kwenye kingo za mto Tighite ili kulinda mazingira na uendelevu wa mto huo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Upandaji miti ukiendelea 
kandokando ya mto Tighite.
------------------------------------------

Mto Tighite ni sehemu ya mfumo wa kiikolojia - unaotiririsha maji kwenye mto mkubwa wa Mara ambao hutiririsha maji kwenye Ziwa Victoria.

Kwa wakazi wa vijiji jirani, mto Tighite ni hazina ya asili, urithi wa vizazi na daraja linalounganisha maisha ya sasa na ya baadaye. Hivyo, kulinda mto huo ni kulinda ‘moyo’ wa vijiji vyao, uhai wa Mto Mara na Ziwa Victoria.

Ndiyo maana siku hiyo, viongozi wa mgodi huo, Jumuiya ya Watumia Maji na vijiji Jirani walishirikiana bega kwa bega kupanda miti ya asili kandokando ya mto huo kijijini Matongo.

“Mbali na kupanda miti ya asili kwenye kingo za mto huu, tutapanda pia miti ya mbao nje ya mita sitini za hifadhi ya mtoni kwa ajili ya matumizi ya kiuchumi ya jamii,” Meneja Mkuu wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko alisema.

Kwa mujibu wa Lyambiko, kazi waliyofanya siku hiyo ni hatua ya awali ya utekelezaji wa programu maalum ya kupamda miti 50,000 kwenye kingo za mto huo katika vijiji 13 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Tigite Chini, Mwita Seri, alisema miti hiyo pia itasaidia kurejesha uoto wa asili na kuimarisha usalama wa maji ya mto huo kwa matumizi ya binadamu, wanyama na viumbe hai wengine.

Wenyeji wanasisitiza kuwa mbali na matumizi mbalimbali ya binadamu ikiwemo kilimo cha umwagiliaji, mto Tighite pia ni chanzo kikuu cha maji kwa mifugo na mimea pori.

Mkazi wa kijiji cha Msege, Sarah Lucas, aliushukuru mgodi huo kwa kuendelea kushirikiana na jamii katika kutunza mazingira, akisema jitihada kama hizo zinasaidia kuleta maendeleo endelevu na kuboresha maisha ya wananchi.

“Miti hii tunayopanda ikikua itasaidia pia kuleta mvua na kuzuia upepo mkali katika maeneo yetu,” Sarah alisema.
Sarah Lucas akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) baada ya kupanda miti.
---------------------------------------

Viongozi wa kijiji cha Matongo, Charles Ryoba (Mwenyekiti) na Faustine Chacha (Afisa Mtendaji), walisema programu hiyo ya upandaji wa miti kandokando ya mto Tighite pia itahamasisha wakazi wa maeneo hayo kujifunza kupanda miti na kutunza mazingira yanayowazunguka.

Aidha, viongozi hao wa kijiji waliahidi kusimamia utunzaji wa miti hiyo iweze kumea na kukua vizuri kwa ajili ya kulinda bioanuwai ya mto huo.

Kwa upande wake, Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi, alisema mgodi huo unashirikiana vizuri na jamii inayouzunguka, ikiwemo Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini iliyobuni wazo la kupanda miti kandokando ya mto huo.

Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa Juni 5 kila mwaka, ikiwa ni jukwaa la kimataifa la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara - unaoendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals, unaamini kuwa uwekezaji kiuchumi unapaswa kuendana na utunzaji wa mazingira kwa vitendo.

Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages