
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka (kulia), Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi na viongozi wengine wakifurahia uzinduzi wa mafunzo kwa wachimbaji wadago wa madini uliofanyika Nyamongo wilayani Tarime, Mara leo Juni 20, 2025.
-------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
Serikali imezindua mafunzo ya siku 14 ya kuvijengea uwezo vikundi 48 vya vijana wachimbaji wadogo wa madini kutoka ukanda wa Nyamongo wilayani Tarime, mkoani Mara.
Mafunzo hayo yataanza kesho Juni 21, 2025, chini ya udhamini wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kwa kushirikiana na North Mara Trust Fund.
Vikundi hivyo vyenye wanachama 2,736 vilikabidhiwa leseni 96 za uchimbaji madini bure na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, mwanzoni mwa Mei 2025.
Hafla ya uzinduzi wa mafunzo hayo imefanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Ingwe - Nyamongo leo, mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi.

Sehemu ya wachimbaji wadogo wa madini waliohudhuria uzinduzi wa mafunzo yao.
-----------------------------------------
Katika hotuba yake, Chikoka amewahimiza vijana hao kuhudhuria mafunzo hayo kikamilifu na kuyazingatia ili yawe muongozo na dira ya shughuli zao za uchimbaji madini.
Sambamba na hayo, amewataka kuepuka migogoro katika vikundi vyao na kutokubali kukatishwa tamaa katika hatua hiyo ambayo aliita safari ya mafanikio.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka (aliyesimama) akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mafunzo hayo.
---------------------------------------
“Kupitia kwenu tunatarajia kuona mabilionea wapya ndani ya Nyamongo. Serikali itakuwa nanyi bega kwa bega, mkiwa na shida pigeni hodi mtafunguliwa na kusikilizwa,” Chikoka amewambia wachimbaji hao.
Aidha, ameishukuru Barrick kwa kuridhia kutoa baadhi ya maeneo yake kwa ajili ya wachimbaji hao, akisema hatua hiyo itasaidia kukomesha tatizo la vijana kuvamia mgodi wa North Mara kwa kisingizio cha kukosa maeneo ya kuchimba madini.

Kwa upande wake, Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa anazofanya kuboresha sekta ya madini nchini.
Uhadi ambaye amemwakilisha Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko, amesema wataendelea kuunga mkono jitihada hizo, na kwamba mafanikio katika mradi huo wa wachimbaji wadogo wa madini yanahitaji ushirikiano kati ya serikali na wadau.

Picha ya pamoja ya viongozi walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa mafunzo hayo.
------------------------------------------
Naye Mkufunzi wa mafunzo hayo, Dkt. Elisante Mshiu, amesema Serikali ya Tanzania inastahili pongezi kubwa kwa kuwa ya kwanza duniani kuanzisha hatua ya kurasimisha wachimbaji wadogo wa madini.
Dkt. Mshiu amesema mafunzo hayo yatahusu elimu ya uchimbaji na uchenjuaji madini, biashara, tabia ya fedha, afya na utunzaji wa mazingira, ushirikiano katika vikundi, sheria na miongozo mbalimbali ya uchimbaji madini.

Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini (mbele) wakiwakilisha wenzao katika picha ya pamoja na viongozi.
------------------------------------------
Nao baadhi ya wachimbaji wadogo wanaokwenda kunufaika na mafunzo hayo, wakiwemo Dominic Daniel, Bedi Elias, Careen John na Ester Max, wameeleza kupokea hatua hiyo kwa furaha, huku wakiomba hatua zilizobaki ziharakishwe ili waanze uchimbaji.
“Tunaishukuru serikali kwa kutuletea mafunzo haya lakini tunaiomba isitucheleweshee hatua zinazofuata ikiwa ni pamoja na kutuonesha maeneo ya kuchimba na kusaidia vitendea kazi vya kisasa,” amesema Ester.
Mafunzo hayo yatafanyika kwa makundi na siku tofauti katika kumbi za shule za sekondari Bwirege, Ingwe, Nyamongo, Nkenge, Kemambo na Julius Kambarage Nyerere zilizopo tarafa ya Ingwe.
No comments:
Post a Comment