NEWS

Wednesday, 11 June 2025

Twiga Minerals yaipa serikali gawio la shilingi bilioni 93.6



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akipokea hundi ya mfano ya gawio la shilingi 93,633,067,640 kutoka Kampuni ya Twiga Minerals jijini Dar es Salaam jana.
-----------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Dar

Kampuni ya Twiga Minerals, ambayo ni kampuni tanzu ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya kimataifa ya madini ya Barrick, imeibuka kuwa miongoni mwa mashirika na taasisi waliochangia kiasi kikubwa cha fedha za gawio kwa serikali mwaka huu.

Twiga Minerals ndiyo kampuni inayoendesha migodi ya dhahabu ya North Mara uliopo Tarime, Mara na Bulyanhulu uliopo Kahama, Shinyanga.

Kampuni hiyo jana ilikuwa miongoni mwa mashirika na taasisi za umma 213 zilizofanya vizuri katika kuchangia gawio kwa serikali kwa kutoa shilingi bilioni 93.6.

Taasisi nyingine zilizofanya vizuri, kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, ni Airtel Tanzania iliyotoa shilingi bilioni 73.9 na Benki ya NMB iliyotoa shilling bilioni 68.1.

Hafla ya mashirika ya umma na taasi za serikali kukabidhi gawio serikalini zilifanyika jijini Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na mgeni rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika hafla hiyo, serikali ilivuna gawio la shilingi trilioni 1.028 kutoka kwa mashirika na taasisi za umma mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 34 ikilinganishwa na shilingi bilioni 767 zilizotolewa mwaka jana.



Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais Samia alitaka mashirika na taasisi za umma kuwajibika kaktika kulinda na kuendeleza uwekezaji wa serikali na kuchangia kikamilifu maendeleo ya kiuchumi.

Alisema mageuzi yanayoshuhudiwa sasa kwenye usimamizi na uendeshaji wa mashirika ya umma yameleta mafanikio, ikiwemo mashirika 11 yaliyokuwa na mtaji hasi kuhamia kwenye mtaji chanya.

Rais Samia alimwagiza Msajili wa Hazina kuwajengea uwezo watendaji wa mashirika na taasisi za umma ili waongeze ubunifu na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Hali kadhalika, alimtaka Msajili wa Hazina kufanya utafiti na kuangalia namna kuongeza ushiriki wa wananchi katika kumiliki mashirika kupitia soko la hisa.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages