
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akizungumza katika Mkutano wa Kwanza wa Wadau wa Maendeleo ya Zao la Tumbaku Mkoa wa Mara, uliofanyika Mugumu, wilayani Serengeti jana.
----------------------------------------
Na Christopher Gamaina, Serengeti
Wakulima na wadau wa tumbaku mkoani Mara wamejadili na kuazimia mikakati ya kuinua uzalishaji wa zao hilo la biashara.
Hatua hiyo imefikiwa katika Mkutano wa Kwanza wa Wadau wa Maendeleo ya Zao la Tumbaku Mkoa wa Mara, ulioandaliwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) na kufanyika Mugumu, wilayani Serengeti jana.

Baadhi ya mapendekezo yaliyopitishwa katika mkutano huo ni usambazaji wa pembejeo kwa wakulima kwa wakati, usimamizi wa ubora wa tumbaku kuanzia shambani na udhibiti wa utoroshaji zao hilo kwanda nje ya nchi.
Pia, wadau hao wa tumbaku waliazimia mikopo ya pembejeo ilipwe kwa wakati, kampuni za ununuzi kutochelewesha malipo kwa wakulima, ulipaji wa tozo za serikali na vyama vya ushirika.

Wadau hao pia waliazimia uwepo mpango wa mafunzo na usambazaji wa teknolojia ili kuwapunguzia wakulima gharama za uendeshaji, pamoja na upandaji wa miti kufidia inayokatwa kwa ajili ya ukaushaji wa zao la tumbaku.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dkt. Khalifan Haule, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kemirembe Lwota kama mgeni rasmi, aliwataka wasambazaji wa mbegu, mbolea na dawa za kuua wadudu kutokuwa na visingizio vya kuchelewesha huduma hizo kwa wakulima.

Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dkt. Khalifan Haule, akifuatilia mada mkutanoni.
--------------------------------------
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, aliziomba benki kufikiria uwezekano wa kupunguza riba za mikopo ya pembejeo kwa wakulima.
Aidha, Meja Gowele aliwataka wanunuzi wa tumbaku kutowapunja wakulima kwenye vipimo vya zao hilo. “Wanunuzi kuweni waaminifu kwenye upimaji wa kilo za tumbaku ili kutowadidimiza wakulima,” alisema.
Meja Gowele alitumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha maofisa kilimo kuwatembelea wakulima, kuwapa ushauri wa kitaalamu na kutambua maeneo yao ya kilimo cha tumbaku ili kujua mahitaji yao halisi ya pembejeo.

Mwenyekiti wa Bodi ya WAMACU Ltd, Momanye Range.
-----------------------------------
Awali, akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya WAMACU Ltd, Momanye Range, alihimiza ushirikiano wa dhati kati ya wakulima wa tumbaku, vyama vya ushirika, serikali, kampuni za ununuzi wa zao hilo na benki zinazotoa mikopo ya pembejeo.
Naye Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye, alitaja wilaya zinazolima zao la tumbaku mkoani Mara kuwa ni Serengeti, Tarime, Rorya na Butiama.

Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye, akisoma risala katika mkutano huo.
No comments:
Post a Comment