
Ngugi wa Thiong’o enzi za uhai
Mwandishi na msomi mashuhuri wa fasihi ya Kiafrika kutoka Kenya, Ngugi wa Thiong’o, alifariki dunia jana Mei 28, 2025 nchini Marekani akiwa na umri wa miaka 87 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Taarifa za kifo cha Ngugi wa Thiong’o zilitolewa na binti yake, Wanjiku wa Ngugi, kupitia ukurasa wake wa Facebook.
Katika taarifa hiyo, Wanjiku aliandika kwa hisia kuwa: “Ni kwa huzuni kubwa tunatangaza kifo cha baba yetu, Ngũgĩ wa Thiong’o, asubuhi ya leo, Jumatano tarehe 28 Mei 2025. Aliishi maisha kamili, alipigana vita nzuri. Kama alivyotamani kabla ya kifo chake, tusherehekee maisha yake na kazi yake.”
Gwiji huyo wa kalamu alitumia maandiko yake kupinga ukoloni wa fikra, akitetea matumizi ya lugha za Kiafrika na uhuru wa kitamaduni.
Ngugi alitambulika sana kwa kazi zake zenye mguso wa kijamii na kiutamaduni kama vile The River Between, A Grain of Wheat, na This Time Tomorrow. Alijenga jina lake kama mmoja wa vinara wa fasihi afrika.
Kifo cha Ngugi wa Thiong’o ni pengo kubwa kwa tasnia ya fasihi, hasa barani Afrika, ambako mchango wake umeacha alama isiyofutika.
No comments:
Post a Comment