NEWS

Tuesday, 22 July 2025

Eliakim Maswi: Mfano wa kuigwa katika kuthamini umuhimu wa waandishi wa habari



Eliakim Maswi

Na Christopher Gamaina

Kutokana na kasi ya maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano duniani, taaluma ya uandishi wa habari inazidi kuhitaji vitendea kazi vya kisasa na bora ili kuhakikisha taarifa zinaandaliwa na kuufikia umma kwa wakati na zikiwa na ubora wa hali ya juu.

Hata hivyo, kumekuwepo na changamoto kubwa kwa waandishi wa habari wengi, hususan katika mikoa ya pembezoni kama Mara, ambapo ukosefu wa vifaa kama kompyuta mpakato (laptop) na kamera umekuwa kikwazo kikubwa katika utendaji wao wa kila siku.

Ni katika muktadha huo, ndipo jina la Eliakim Maswi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, limeibuka miongoni mwa viongozi na wadau wachache wanaotambua mchango muhimu wa wanahabari katika kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii, sambamba na kuweka msukumo wa kuimarisha uwajibikaji wa serikali kwa wananchi.

Kupitia mfuko wake binafsi, Maswi ametumia zaidi ya shilingi milioni 11.4 kuwanunulia laptop waandishi wa habari 14 wa mkoani Mara, kwa lengo la kurahisisha kazi zao na kuongeza ufanisi wa kiutendaji.

Huu ni moyo wa kipekee wa uzalendo na upendo kwa taaluma ya habari. Si tu kwamba msaada huu umekuja wakati mwafaka, bali pia umebeba ujumbe mkubwa kwa wadau wengine wa maendeleo na mawasiliano nchini - kuwa waandishi wa habari ni nguzo muhimu ya maendeleo endelevu, na wanastahili kuungwa mkono kwa vitendo, si kwa maneno tu.

Maswi ambaye ni mzaliwa wa wilaya ya Tarime, mkoani Mara, ameonesha dhamira ya dhati ya kurudisha kwa jamii yake alichojaliwa na Mungu kwa njia ya kuwajali waandishi wa habari wanaojituma kwa bidii katika mazingira magumu.

Ametambua kuwa katika dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa wa kimitandao na habari za kidijitali, ubora wa kazi ya mwandishi wa habari umefungamana moja kwa moja na upatikanaji wa vifaa vya kisasa.

Wengi miongoni mwa wanahabari waliofaidika na msaada huo hawakusita kueleza furaha yao na namna vifaa hivyo vitakavyoongeza ari ya kazi.

Laptop hizo si tu zitarahisisha uandishi, uhariri na kutuma habari kwa wakati, bali pia zitawapunguzia gharama za kuazima au kutumia vifaa vya watu wengine ambavyo mara nyingi huathiri ratiba na ubora wa kazi.

Katika jamii zetu ambako mara nyingine wanahabari huonekana kama kundi lisilo na uhitaji wa msaada wa moja kwa moja, hatua kama hii ya Maswi inafungua ukurasa mpya wa fikra - kwamba kuwaunga mkono waandishi wa habari ni kuunga mkono maendeleo ya jamii nzima.

Waandishi bora, waliowezeshwa na vifaa bora, huweza kusimamia kwa karibu maendeleo ya jamii na kufichua changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.

Maswi hakufanya haya kwa kutafuta sifa. Kama mdau wa muda mrefu wa sekta ya habari, siku zote amekuwa mstari wa mbele kuwasikiliza na kushirikiana na wanahabari katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Kwa hakika, hiki ni kielelezo dhahiri kuwa Maswi ni kiongozi mwenye maono mapana na anayethamini uwazi, haki na umuhimu wa upashanaji sahihi wa habari.

Ni wakati sasa kwa viongozi wengine, wadau wa habari, taasisi na mashirika binafsi kujifunza kutoka kwa Maswi kwamba kuwekeza kwa waandishi wa habari si kazi ya serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja anayetamani kuona taifa likiendelea katika msingi wa taarifa sahihi, zinazojenga na kuimarisha uwajibikaji.

Tunampongeza Eliakim Maswi kwa moyo huu wa kipekee. Tunaipongeza pia Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara chini ya Mwenyekiti wake, Jacob Mugini, kwa kuendelea kuonesha umoja na mshikamano wao.

Matarajio ya wengi ni kwamba waandishi wa habari waliopata msaada wa laptop hizo watazitumia kutekeleza majikumu yao kwa weledi na kuwa chachu ya kuimarisha zaidi kazi zao.

Mungu ambariki Eliakim Maswi na aendelee kuwa mwanga wa matumaini kwa waandishi wa habari mkoani Mara na Tanzania kwa ujumla.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages