
Janeth Antony Mtiba
Na Mwandishi Maalumu
Historia mpya imeandikwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tarime Mjini, baada ya binti mwenye umri mdogo zaidi kujitokeza kutia nia ya ubunge katika jimbo hilo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Janeth Antony Mtiba, ndiye mwenye umri mdogo zaidi – miaka 30, katika makada 14 wa CCM waliojitokeza kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea kiti cha ubunge jimbo la Tarime Mjini katika uchaguzi huo.
Kada huyo kijana anasema uamuzi wake wa kujitokeza kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM katika kinyang’anyiro cha ubunge umetokana na wito wa ndani alionao wa kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo.
"Nimeamua kuchukua fomu kutokana na wito uliopo ndani yangu wa kuwatumikia wananchi wa jimbo la Tarime Mjini,” alisisitiza Janeth katika mahojiano na Sauti ya Mara na kuongeza kuwa wakati umefika kwa damu changa kujitokeza kusaidia kuharakisha maendeleo ya jimbo hilo la mkoani Mara.
Janeth ambaye pia ni Mwanzilishi wa Taasisi ya Samia Golden Girls inayolenga kuwawezesha mabinti kielimu na kiuchumi, aliweka wazi kuwa anachochewa na kasi ya utendaji kazi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mfano wa uongozi bora, jumuishi na wa vitendo.
“Nimevutiwa na kasi alianayo Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anahitaji mwakilishi wa jimbo atakaeendana na kasi yake ya kuhakikisha wananchi wanapatiwa kwa wakati maendeleo yanayohitajika, na mtu mwenyewe ni mimi Janeth Antony Mtiba,” alisema kwa kujiamini.
Mbali na msukumo wa uongozi bora wa Rais Samia, Janeth alisema amewekeza muda mwingi katika kufanya tafiti ili kutambua changamoto halisi zinazowakabili wakazi wa Tarime Mjini, hususan katika sekta za elimu, afya na uchumi.
Anaamini kuwa uongozi wa kisasa unaotegemea takwimu, utafiti na maono thabiti ndio unaohitajika kulivusha jimbo hilo katika zama mpya za maendeleo endelevu.
“Wito huu umetokana na kutumia muda mwingi wa kufanya tafiti ili kubaini changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta za elimu, afya na Uchumi - na hatimaye kuifanya Tarime Mjini kuwa lango na mhimili wa maendeleo endelevu,” alisisitia Janeth
Wakati vikao vya maamuzi ndani ya CCM ngazi ya taifa vikitarajiwa kuweka hadharani majina ya wanachama watakaochuana kwenye kura za maoni za ubunge siku chache zijazo, jina la Janeth Mtiba tayari limekuwa gumzo kwenye vijiwe vya kisiasa Tarime Mjini.
Jina lake limekuwa limeibua mjadala mpana pia kwenye mitandao ya kijamii na vikao vya vijana, hasa kutokana na ujasiri wake, umri wake mdogo na dira aliyonayo kwa mustakabali wa jimbo hilo.
Kwa kuzingatia hali ya sasa ya kisiasa, kuibuka kwa wagombea vijana kama Janeth Mtiba kunatoa taswira ya mabadiliko ndani ya siasa za Tanzania – ambapo ujasiri, nguvu ya hoja na maono ya kushughulikia changamoto za wananchi vinazidi kuchukua nafasi kama kipimo cha uongozi unaohitajika katika jamii.
No comments:
Post a Comment