NEWS

Tuesday, 22 July 2025

TANAPA yasisitiza watalii kutoshuka kwenye magari maeneo yasiyoruhusiwa hifadhini



Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TANAPA, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Catherine Mbena.
---------------------------------------

Na Mwandishi Wetu

Watalii wamekumbushwa kuzingatia Sheria, Kanunni na Taratibu za Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), ikiwa ni pamoja na kutoshuka kwenye magari katika maeneo yasiyoruhusiwa hifadhini.

TANAPA imetoa msisitizo huo kufuatia picha jongefu na za mnato zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha watalii wameshuka kwenye magari eneo la Kogatende kivuko namba nne katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Tukio hilo lilitokea Julai 21, 2025 katika eneo hilo ambalo ni miongoni mwa maeneo ambayo watalii hawaruhusiwi kushuka kwenye magari.

Hata hivyo, askari wa TANAPA walifika eneo hilo na kuwaelekeza watalii hao kurudi kwenye magari yao, kwani kitendo cha kushuka kinaharibu utaratibu mzima wa misafara ya wanyamapori.

Taarifa hiyo ya TANAPA iliongeza kuwa watalii wanaposhuka kwenye magari maeneo yasiyoruhusiwa pia wanaharibu mazingira na kuhatarisha usalama wao.

“TANAPA imeshayabaini magari yote yaliyohusika katika kadhia hiyo na hatua kali zimeanza kuchukuliwa dhidi ya waongoza watalii hao,” ilihitimisha taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TANAPA, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Catherine Mbena.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages