NEWS

Saturday, 19 July 2025

RC Mtambi aiona Mara yenye mabilionea wengi siku za usoni



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, akizungumza katika mkutano maalum na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma, Julai 18, 2025.
------------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu, Dodoma

Mkoa wa Mara upo katika nafasi nzuri ya kuwa na mabilionea wengi katika siku za usoni, Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Evans Alfred Mtambi amesema.

Kanali Mtambi alisema hayo mbele ya waandishi wa habari jijiji Dodoma, jana Ijumaa wakati akitangaza mafanikio yaliyopatikana mkoani humo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alisema wakazi wa mkoa huo wameanza kuchangamkia fursa lukuki za maendeleo zilizopo, zikiwemo za utajiri mkubwa wa madini, utalii, uvuvi, kilimo na ufugaji ambazo zimeanza kutumika vizuri kwa maendeleo ya kiuchumi.

Alitoa mfano wa mradi wa kuwezesha wachimbaji wadogo wa madini - ambao hivi karibuni walipewa leseni 48 za uchimbaji madini, mradi ambao umewezeshwa na Serikali ya Tanzania kwa uhisrikiano wa karibu na Kampuni ya Barrick kupitia mgodi wake wa dhahabu wa North Mara.

Mradi huo ambao Kanali Mtambi alisema ni mfano sio tu kwa Tanzania bali kwa dunia, unalenga vijana na wanawake kutoka vijiji 13 vinavyozungka Mgodi wa Dhahbau wa North Mara, ambao unaendeshwa na Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

“Uwezeshaji wa walengwa ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya Mining for Brighter Tomorrow (MBT) ambao mkoa wa Mara ni ‘benchmark point’. Ni mradi wa kwanza kufanyika duniani,” alisema Kanali Mtambi.

Alisema mradi huo sio wa patapotea kwa sababu utafiti makini unafanyika ili kuwawezesha wote wanaopewa leseni kuchimba dhahabu badala ya uchimbaji wa kubahatisha. “Tunatarajia kuwa na mabilionea wa siku za usoni,” alisisitiza kiongozi huyo wa mkoa.

Kanali Mtambi alisema mkoa wa Mara umezalisha dhahabu tani 58.9 yenye thamani ya shilingi trilioni 6.9, jambo ambalo limewezesha taifa kupata madhuhuli ya shilingi bilioni 668.

“Kwa mikakati tuliyonayo, mkoa wa Mara utaupita mkoa wa Geita katika sekta ya madini,” alisema Kanali Mtambi.

Aliongeza kuwa miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 33.8 imetekelezwa chini ya Mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) katika sekta ya madini mkoani humo.

Mgodi wa North Mara unatajwa kuwa kinara wa kuchangia maendeleo kupitia mpango wake wa CSR katika mkoa huo, huku Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vjijini) ikiwa mnufaika mkubwa.

Mfano, Aprili 29, mwaka huu, mgodi wa North Mara ulizindua rasmi awamu nyingine ya utekelezaji wa miradi 19 ya barabara na mmoja wa maji, ikiwa ni miongoni mwa miradi ya kijamii 101 itakayotekelezwa kwa gharama ya shilingi zaidi ya bilioni tisa za CSR zilizotolewa na mgodi huo kutokana na uzalishaji wa mwaka 2023.

Aidha, tayari mgodi huo umetenga kiasi kingine cha shilingi zaidi ya bilioni 4.687 za CSR kutokana na uzalishaji wa mwaka 2024 kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi ya kijamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

Kanali Mtambi alisema wakazi wa Mara wana kila sababu ya kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuupatia mkoa huo fedha nyingi kwa ajili ya miradi mingi, ikiwemo ya kimkakati.

Miradi hiyo ni pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Kwangwa, Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kilichopo Butiama, pamoja na upanuzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege Musoma.

Kanali Mtambi aliahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa serikali na wadau wote wa maendeleo katika kuijenga Mara iliyo boara zaidi.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages