NEWS

Saturday, 5 July 2025

Wakulima Serengeti waimiminia Pamoja Tuwalishe shukrani wakiadhimisha Siku ya Mkulima Shambani



Viongozi (waliovaa jaketi za kijani) na baadhi ya wakulima wakiwa tayari kwa tukio la makabidhiano ya pembejeo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mkulima Sahambani yaliyofanyika katika kijiji cha Nyansurumunti wilayani Serengeti, Mara, Julai 2, 2025.
------------------------------------------

Na Christopher Gamaina, Serengeti

Julai 2, 2025, ilikuwa siku ya kipekee, yenye furaha na matumaini kwa wakulima katika wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, hususan katika kijiji cha Nyansurumunti katani Kisaka, yalipofanyika Maadhimisho ya Siku ya Mkulima Shambani.

Mamia ya wakulima - wanawake kwa wanaume kutoka vijiji na kata jirani, walijitokeza kushiriki maadhimisho hayo - ambayo si tu yaliwakutanisha, bali pia yaliwakumbusha umuhimu na thamani yao katika ustawi wa jamii na taifa.

Ndiyo siku mbayo wakulima hao walimimina shukrani zao kwa Mradi wa Pamoja Tuwalishe unaotekelezwa na Shirika la Global Communities, kwa jitihada kubwa za kuwawezesha kuendesha kilimo cha kisasa chenye tija na endelevu.
Sehemu ya wakulima wakifuatilia
tukio katika maadhimisho hayo.
----------------------------------------

Wakulima hao waliutaja Mradi wa Pamoja Tuwalishe kama mkombozi wao kutokana na kuwajengea uwezo wa kuinua uzalishaji ili kujitegemea kwa chakula na kipato.

Kupitia mradi huo unaofadhiliwa na mjasiriamali wa nchini Marekani, Rick Steves, wakulima wanapewa elimu ya kanuni bora za kilimo cha kisasa na endelevu cha mazao mbalimbali, kama vile mahindi, alizeti na maharage.

Aidha, wanapewa misaada ya pembejeo, hususan mbegu bora, mbolea na viuatilifu vya kuua wadudu waharibifu wa mazao mashambani.

Mkulima, Janet Bhoke Mwita kutoka kijiji cha Nyiboko, alitoa ushuhuda mbele ya Mara Online News kwenye viwanja vya maadhimisho hayo, akisema “Tumepata mafanikio makubwa katika shughuli zetu za kilimo kutokana na ujuzi na misaada ya pembejeo tuliyopata kutoka mradi wa Pamoja Tuwalishe.”
Janet Bhoke Mwita akizungumza na Mara Online News pembezo mwa shamba darasa la alizeti kijijini Nyansurumunti.
----------------------------------------

Mashamba darasa ya mazao ya alizeti na mahindi yaliyolimwa na Kikundi cha Umoja wa Vijana katika kijiji cha Nyansurumunti chini ya usimamizi wa wataalamu na ufadhili kutoka Pamoja Tuwalishe na kampuni ya mbegu ya SEED CO, yanatajwa kuhamasisha wananchi wengi kujiunga kwenye vikundi vya kilimo ili kunufaika na maarifa yanayotolewa na wadau hao wa kilimo.

Juma Limbu, mkulima mkongwe katika kijiji cha Nyansurumunti, anasema kama si mashamba darasa hayo, asingejua kuwa mbegu bora za mahindi zinaweza kunizalishia magunia zaidi ya 20 kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari moja. “Global Communities kupitia mradi wa Pamoja Tuwalishe na SEED CO wametufungua macho, sasa tunaona mwanga,” alisema.

Mkulima Juma Limbu akizungumza na Mara Online News kijijini Nyansurumunti.
--------------------------------------

Mkulima mwingine na mkazi wa kata ya Kisaka, Rhoda Deus Marwa, alishukuru akisema kwamba kupitia Mradi wa Pamoja Tuwalishe, wamefundishwa namna ya kupanda kwa mistari, kutumia mbolea kwa kipimo sahihi na kutunza mazao mashambani.

Wakulima wengi wanasema mavuno ya mazao yao kwa sasa yameongezeka kwa zaidi ya mara tatu baada ya kupata elimu kutoka kwa maofisa wa Pamoja Tuwalishe na SEED CO, ambapo sasa wanajua kutumia mbinu bora - kuanzia matumizi sahihi ya mbegu na mbolea - hadi usimamizi wa mashamba kulingana na mabadiliko ya tabianchi.

Mkulima kijana na mkazi wa kijiji cha Nyansurumunti, Ibra Mwita, alisema alizoea kulima kienyeji, lakini sasa anajua kuwa kilimo ni sayansi na sayansi hiyo anaifanyia kazi kwa vitendo. “Nawashukuru sana wadau wetu kutoka Pamoja Tuwalishe na SEED CO kwa kutuwezesha,” alisema.


Sehemu nyingine ya wakulima waliohudhuria maadhimisho hayo kijijini Nyansurumunti.
-----------------------------------------

Naye mgeni rasmi katika maadhimishi hayo ya Siku ya Mkulima Shambani, Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Serengeti, Bwenda Bainga, alilishukuru Shirika la Global Communities linalotekeleza Mradi wa Pamoja Tuwalishe kwa kushirikiana na SEED CO, na kuomba huduma hizo zisambazwe kwenye maeneo mengi ili kunufaisha wakulima wengi zaidi.

Aidha, Bainga ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, aliwataka wakulima waliopata elimu ya kilimo cha kisasa chenye tija kuizingatia kwa vitendo, lakini pia kutokuwa wachoyo wa kuifikisha kwa wengine ambao hawakupata bahati ya kuipata.

“Serikali na wafadhili wanatumia gharama kubwa kutoa elimu, ikiwa ni pamoja na kuendesha mashamba darasa, hivyo kila aliyepata ujuzi auzingatie na kuusambaza kwa wengine,” alisisitiza.
Bainga akizungumza katika
maadhimisho hayo.
-----------------------------------------

Vilevile, Bainga aliwakumbusha wataalamu wa kilimo ngazi za kijiji na kata kuwaelekeza wakulima utaratibu wa kujisajili kwa ajili ya kupata namba za kununua mbolea ya ruzuku ambayo serikali inachangia gharama, huku akiitaka SEED CO kuhakikisha mbegu zinawafikia wakulima kwa wakati.

Bainga alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuhimiza wazazi na walezi kuwa tayari kuchangia shakula cha wanafunzi shuleni ili kuongeza ufaulu na kupunguza utoro.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Hillary Dashina kutoka Global Communities, alisema wanaelimisha wakulima kanuni bora za kilimo cha kisasa na kuwapatia pembejeo ili kuimarisha usalama wa chakula ngazi ya kaya na taifa kwa ujumla.
Hillary Dashina kutoka Global Communities akizungumza na Mara Online News kijijini Nyansurumunti.
--------------------------------------------

Dashina aliongeza kuwa dhamira yao ni kuhakikisha kila mkulima anapata elimu sahihi ya kilimo, pembejeo bora na ufuatiliaji wa karibu ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kuondoa njaa na umskini kwenye jamii.

Shirika la Global Communities lenye makao makuu mkoani Dodoma, linatekeleza Mradi wa Pamoja Tuwalishe katika mkoa wa Mara, ambapo Dashina alisema hadi sasa limeshawafikia wakulima 800 katika wilaya za Butiama na Musoma, na katika wilaya za Serengeti na Tarime limeshawafikia wakulima 500. “Asilimia 65 ya wakulima tuliowafikia ni wanawake,” alibainisha.

Dashina alihitimisha kwa kueleza kuwa fahari yao ni kuona mkulima wa kawaida anainuka kutoka kwenye umaskini na njaa - hadi kuwa na uzalishaji wenye tija na kujitegemea kwa chakula na kipato cha uhakika.


Afisa Masoko wa SEED CO, Mbayani Terito, akionesha alizeti ilivyostawi kwenye shamba darasa kijijini Nyansurumunti.
------------------------------------------

Kwa upande wake, Afisa Masoko wa SEED CO, Mbayani Terito, alisema katika mpango huo wa kuwajengea wakulima uwezo, pia wamekuwa wakishirikiana na Mradi wa Pamoja Tuwalishe kusambaza pembejeo, zikiwemo mbegu na mbolea kwa wakulima.

Maadhimisho hayo ya Siku ya Mkulima Shambani yalihitimishwa kwa mgeni rasmi kukabidhi msaada wa mbegu na mbolea bora, sambamba na zawadi za fulana na vyeti vya upimaji udongo kwa vikundi vya wakulima.
Ugawaji wa pembejeo na zawadi ukiendelea. (Picha zote na Mara Online News)
-----------------------------------------

Msaada wa pembejeo na zawadi hizo vilitolewa na Global Communities kupitia Mradi wa Pamoja Tuwalishe na SEED CO - kama sehemu ya kuvihamasisha vikundi hivyo vya wakulima kuzalisha kwa tija zaidi.

Maadhimisho hayo pia yalihudhuriwa na Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Butiama, Fred Kisika, Mtaalamu wa Kilimo kutoka Global Communities, Dkt. Amithay Kuhanda na Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Vikundi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Hungila Michael, miongoni mwa viongozi wengine.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages