
Esther Matiko
Na Mwandishi Wetu, Mara
Wanawake wanne, wakiwemo wawili wapya na wengine wawili ambao wamekuwa wabunge kwa mihula mitatu mfululizo, wameteuliwa na chama tawala - CCM kuwa wagombea wake wa ubunge katika majimbo manne ya mkoani Mara kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Wabunge hao na majimbo ya uchaguzi wanayogombea yakiwa kwenye mabano ni Esther Matiko (Tarime Mjini), Esther Bulaya (Bunda mjini), Mgore Kigera (Musoma mjini) na Mary Daniel (Serengeti).
Matiko na Bulaya ambao kila mmoja amekuwa mbunge wa viti maalum kwa mihula miwili na mbunge wa jimbo kwa mhula mmoja, walihama chama cha upinzani - CHADEMA na kujiunga na CCM hivi karibuni kisha kujitupa kwenye kura za maoni za ubunge ndani ya chama hicho tawala na hatimaye kufanikiwa kupata uteuzi huo.

Esther Bulaya
Uteuzi wa wawili hao ambao ni maarufu katika medani za siasa nchini, umeandika historia mpya ya kuteuliwa wakiwa watia nia walioshika nafasi ya tatu katika kura za maoni kwenye majimbo yao.
Katika jimbo la Serengeti, Mary Daniel ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Mara, ameibuka ghafla kama mwanasiasa mchanga mwenye mvuto mkubwa kwa makundi yote ya wananchi.
Mshangao mkubwa mwingine ni uteuzi wa Mgore Kigera kugombea ubunge wa jimbo la Musoma Mjini. Huyu pia ni Mjumbe wa Baraza la Wazazi CCM Taifa anayeheshimika kwa misimamo na uwezo wa kujenga hoja. Wengi wanamuona kama chaguo sahihi kwa mji wa kihistoria wa Musoma.

Mgore Kigera (kushoto) na Mary Daniel
Wanawake hao wanne wameonesha uthubutu wa kuwa mstari wa mbele katika mapambano hayo katika mkoa wa Mara ambao siku zote unatajwa kuwa na ushindani mkali wa kisiasa.
Je, wataweza kuhimili mikikimikiki ya kampeni za Uchaguzi Mkuu? Hilo ni swali litakalopata jibu kadri Oktoba 2025 inavyokaribia.
No comments:
Post a Comment