NEWS

Monday, 25 August 2025

Kiongozi Mbio za Mwenge wa Uhuru aimwagia sifa Kampuni ya Barrick



Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, akizindua upanuzi wa mradi wa chanzo cha maji unaotekelezwa kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele na Meneja Mkuu wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko (katikati).
----------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu, Tarime

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, ameipongeza Kampuni ya Barrick kwa kuendelea kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini kupitia uwekezaji wake katika migodi ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu.

“Barrick ni miongoni mwa wawekezaji wanaofanya vizuri nchini. Kwa dhati ya moyo wangu ninamshukuru na kumpongeza sana mwekezaji huyu - ana dhamira ya kuhakikisha taifa letu linapata maendeleo,” Ussi alisema alipokwenda kuzindua mradi wa upanuzi wa chanzo cha maji katika mgodi wa North Mara wiki iliyopita.

Alisema mradi huo ambao utagharimu shilingi bilioni 2.6 zilizotengwa na Barrick North Mara kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na kampuni hiyo kuunga juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kuleta mageuzi makubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Mradi huo unalenga kusambaza maji safi na salama kwa maelfu ya wakazi wa vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi huo uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

“Kwa kweli wananchi wamepata faraja na wanaendelea kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kutokana na maendeleo makubwa mabayo yamefanyika,” alisema Ussi na kuongeza:

“Leo pia nimeona mradi wa CSR wa zahanati katika kijiji cha Mangucha. Na siyo hapa tu [Tarime], Barrick wamejenga pia soko la kisasa kule Msalala (mkoani Shinyanga).”

Mapema, Mwenge huo wa Uhuru ulizuru katika kata ya Nyanungu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa zahanati ya kisasa ya kijiji cha Mangucha unatekeleza kutokana na mamilioni ya fedha za CSR Barrick North Mara.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi (kushoto), akiweka jiwe la msingi katika Zahanati ya Kijiji cha Mangucha wiki iliyopita. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele na Meneja Uhusiano wa mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi (kulia).
-----------------------------------------

Ussi aliipongeza Barrick kwa kuwa mfano mzuri wa kutoa mabilioni ya fedha za CSR kwa wakati kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi katika maeneo inakoendesha migodi yake.

Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, alisema miradi hiyo pia ni matunda ya ushirikiano na uhusiano mzuri uliopo kati ya migodi inayoendeshwa na kampuni hiyo na wananchi wanaoizunguka.

Hivyo, Ussi aliahidi kuwa balozi wa kazi nzuri inayofanywa na Barrick kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Nitakuwa balozi kwa kumfikishia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ushuhuda wa kazi nzuri inayofanywa na kampuni ya Barrick,” alisema na kumpongeza Rais Samia kwa kujenga mazingira bora ya uwekezaji nchini.

Kwa upande mwingine, Ussi aliipongeza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara kwa kuonesha umahiri mkubwa katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji.

“Hatukuona changamoto yoyote ya miradi ya maji tangu tuingie katika mkoa huu - na tumeridhika kwa asilimia 100 juu ya utekelezaji wa miradi hii,” alisema Ussi.

Awali, Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mohamed Mtopa, alimweleza kiongozi huyo wa mbio za Mwenge Uhuru kwamba mwanzoni chanzo hicho cha maji kilichopo katika mgodi wa North Mara kilisanifiwa kuhudumia wakazi 27,742 wa vijiji vinne - Nyangoto, Matongo, Mjini Kati na Nyabichune.

Lakini kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji katika vijiji saba vinavyozunguka mgodi wa North Mara, chanzo hicho kilisanifiwa upya kwa lengo la kuhudumia wakazi 125,566 katika vijiji saba - Kewanja, Genkuru, Nyamwaga, Nyakunguru, Kerende, Msege na Komarera, na hivyo kufanya idadi ya vijiji vinavyolengwa kufikia 11 ambavyo vinazunguka mgodi wa North Mara.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mtopa, mradi huo ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 80, utaongeza uzalishaji kutoka lita 2,314,000 za sasa hadi 10,213,000 na hivyo kufikia lengo la serikali la mwaka 2020-2025 la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi waishio vijijini.

Mradi huo unatarajiwa kuwaondolea wakazi wa vijiji husika adha waliyokuwa nayo ya kutumia muda mrefu kutafuta maji, ambapo sasa watapata muda wa kujielekeza kwenye shughuli za uzalishani mali na kukuza uchumi wao.

Barrick inaendesha migodi ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages