
Prof. Sospeter Muhongo
Na Mwandishi Wetu, Mara
Mbali na wanawake wanne walioteuliwa kugombea ubunge katika majimbo manne mkoani Mara, Chama Cha Mapinduzi (CCM) pia kimepandisha joto la uchaguzi kwa kuteua wanaume sita kugombea ubunge katika majimbo sita ya mkoa huo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Wanaume hao ni Profesa Sospeter Muhongo, gwiji wa jiolojia ambaye anatetea ubunge wa jimbo la Musoma Vijijini. kiongozi huyu ambaye anaheshimika kwa weledi wake wa kitaalamu na ujasiri bungeni, anarudi ulingoni akiwa na msimamo usioyumba katika masuala yenye maslahi mapana ya taifa.
Katika jimbo la Butiama, nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, CCM imemkabidhi kijiti Dkt. Wilson Mahera, daktari bingwa na mwanasiasa aliyedhamiria kuleta mageuzi chanya ya kijamii na kiuchumi katika ardhi hiyo ya kihistoria.

Dkt. Wilson Mahera
Wananchi wa Butiama wana shauku kubwa ya kuona namna Dkt. Mahera atakavyolinda heshima ya urithi wa Mwalimu Nyerere kupitia sera na utendaji.
Chaguo la CCM kwa upande wa jimbpo la Rorya ni Jafari Wambura Chege. Anajulikana kwa ushawishi mkubwa alio nao kwa wananchi na uzoefu katika sekta ya maendeleo ya jamii. Anatazamiwa kuwa kiongozi atakayevunja mwiko wa siasa za mazoea katika eneo hilo lenye historia ya ushindani mkali wa kisiasa.

Jafari Wambura Chege
Mwita Waitara yeye amerejeshwa kugombea jimbo la Tarime Vijijini. Waitara ambaye ni mwanasiasa mwenye historia ya kuvuka kutoka upinzani hadi CCM, anajulikana kwa uhodari wa kujibu mapigo kisiasa na kujenga hoja.

Mwita Waitara
Boniphace Getere, ambaye amekuwa Mbunge wa Bunda Vijijini kwa mihula miwili mfululizo, ameaminiwa tena na CCM kutetea kiti cha ubunge. Getere anafahamika kwa kauli kali lakini zenye ujumbe mzito, na ni mmoja wa wanasiasa waliobobea katika siasa za kimkakati.

Boniphace Getere
Kwingineko katika jimbo la Mwibara, jina la Kangi Lugola linarejea tena kwenye medani za siasa. Kangi ambaye pia ni maarufu kwa mbwembwe bungeni, amewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

No comments:
Post a Comment