NEWS

Wednesday, 13 August 2025

Chichake atoa milioni 10/- kuchangia gharama za kampeni za CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025



Kada wa CCM, Nicolaus Chichake.

Na Mwandishi Wetu, Dar

Mjasiriamali na msomi wa chuo kikuu, Nicolaus Chichake, ni miongoni mwa Watanzania waliowiwa na kujitokeza katika harambee ya kuchangia gharama za kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini Oktoba 29, 2025.

Katika harambee hiyo iliyozinduliwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan jijini Dar es Salaam jana Agosti 12, 2025, Chichake alipewa nafasi akatangaza kuchangia shilingi milioni 10.

Chichake ambaye ni mmoja wa makada wa CCM waliotia nia ya ubunge jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara mwaka huu, alitoa mchango huo kuunga mkono juhudi za chama hicho katika kuhakikisha kinapata ushindi wa kishindo kwa wagombea wake kote nchini.

Chichake anaamini CCM ni chama kinachobeba matumaini ya Watanzania wengi, hivyo yeye kama kijana na mzalendo wa kweli, ameona ana wajibu wa kuchangia jitihada hizo kwa moyo mkunjufu.

Kitendo hicho cha Chichake kimewavutia wengi na kuibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii, ambapo baadhi wanakiona kama dalili ya uaminifu na uzalendo, huku wengine wakikitafsiri kama hatua ya kujijenga kisiasa kwa chaguzi zijazo.

Katika hafla ya uzinduzi wa harambee hiyo inayoendelea, Chama Cha Mapinduzi kilifanikiwa kukusanya shilingi bilioni 86.3, fedha taslimu zikiwa bilioni 56.31 na ahadi bilioni 30.2.

Kati ya kiasi hicho cha fedha hizo, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia, alichangia shilingi milioni 100, huku Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akichangia shilingi milioni 50, miongoni mwa wengine.

Lengo la CCM ni kukusanya shilingi bilioni 100 ambazo zitakiwezesha kuzunguka maeneo mbalimbali nchini kujinadi kwa wananchi.


Dkt. Samia (katikati), Dkt. Mwinyi (kushoto) na Balozi Dkt. Nchimbi (kulia) wakipiga makofi kufurahia jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa harambee hiyo.
---------------------------------------

Akizungumza baada ya uzinduzi na uchangiaji huo wa jana, Dkt. Samia aliwashukuru wote waliochangia na watakaoendelea kuchangia kwa ajili ya kuwezesha kampeni za chama hicho.

“Kutoa ni moyo si utajiri, michango yenu itatuwezesha kufikia lengo na tutaweza kukamilisha kampeni zetu salama,” alisema Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa.

Dkt. Samia alitumia nafasi hiyo pia kuwahamasisha wote wanaotaka kukichangia chama hicho, wakiwamo Diaspora (Watanzania wanaoishi nje ya nchi) kutosita kufanya hivyo kupitia utaratibu uliowekwa.

Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, alisema michango hiyo inaendelea mpaka Agosti 27, 2025.

Dkt. Samia ndiye mteule wa CCM wa kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa na mgombea mwenza, Balozi Dkt. Nchimbi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages