NEWS

Wednesday, 13 August 2025

Serikali yasaini mikataba minne kuimarisha utalii



Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana (aliyekaa) akishuhudia hafla ya utiaaji saini ya mikataba hiyo jana.
-------------------------------------

Na Mwandishi Wetu

Mikataba minne ya uwekezaji wa dola za Marekani milioni 158.8 unaolenga kuimarisha sekta ya utalii nchini ilitiwa saini jana jijini Dar es Salaam na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia utaratibu wa Uwekezaji Mahiri (SWICA).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii, uwekezaji huo unalenga vitalu vya Burko Open Area (Monduli-Arusha), Selous MHJ1, Selous MHJ2 na Selous ML1 (Liwale-Lindi).

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, alisema Mpango wa SWICA unatoa fursa kwa mwekezaji kufanya shughuli za utalii wa picha na uwindaji wa kitalii ndani ya kitalu kimoja tofauti na utaratibu uliozoeleeka ambao mwekezaji kwa kiasi kikubwa hufanya shughuli za uwindaji pekee.

Alisema uwekezaji huo unatarajiwa kuingiza dola za Marekani milioni 281.5 (shilingi bilioni 719), ikiwa ni wastani wa shilingi bilioni 36 kila mwaka kwa kipindi cha miaka 20.

Inatarajiwa kwamba wananchi wanaoishi kuzunguka maeneo hayo nao watanufaika kwa ajira na miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa zahanati, miradi ya maji na ujenzi wa madarasa miradi yote ikikadiriwa kugharimu shilingi bilioni 4.6 ambazo ni sawa na dola za Marekani milioni 1.8, Waziri alisema.

Haya ni mafanikio makubwa kwa sekta ya utalii. Tumeanza kutafsiri vizuri malengo ya Dira ya Maendeleo 2050 ya kuipaisha Tanzania kuwa kinara wa utalii barani Afrika, alisema Waziri.

Hafla hiyo fupi ya kusainiwa mikataba ilihudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu wa wizara na taasisi zilizo chini yake.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages