NEWS

Thursday, 14 August 2025

RC Mara awaalika wananchi mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2025 kesho



Mkuu wa Mkoa wa Mara, 
Kanali Evans Alfred Mtambi.
----------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma

Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 zitawasili mkoani Mara kesho Agosti 15, ambapo utatembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi, kufungua na kuzindua miradi 68 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 26,547,598,285 katika halmashauri zote tisa za mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma jana, Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, alisema Mwenge huo utatokea mkoa wa Simiyu na kupokewa katika Halmashauri ya Mji Bunda kesho Agosti 15 kwa ajili ya kukimbizwa umbali wa kilomita 1,123 hadi Agosti 23, 2025 kisha kuelekea mkoani Mwanza siku inayofuata.

“Ninawakaribisha wananchi wote wa Mkoa wa Mara kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru katika Uwanja wa Shule ya Msingi Balili, Halmashauri ya Mji wa Bunda keshokutwa [kesho] kuanzia saa 12 asubuhi,” alisema Kanali Mtambi.

Ratiba inaonesha kuwa Mwenge wa Uhuru 2025 utakimbizwa katika Halmashauri ya Mji wa Bunda kesho Agosti 15, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama (Agosti 16), Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (Agosti 17) na Halmashauri ya Manispaa ya Musoma (Agosti 18, 2025).

Halmashauri ya Wilaya ya Rorya (Agosti 19), Halmashauri ya Mji wa Tarime (Agosti 20), Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Agosti 21), Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti (Agosti 22) na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda (Agosti 23, 2025).

Kanali Mtambi alisema ukiwa Mara, Mwenge wa Uhuru ukiwa wilayani Butiama utatembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambapo kama ilivyo kawaida utawasha Mwenge wa Mwitongo kwa mara ya 61 tangu Mbio za Mwenge wa Uhuru zilipoanzishwa mwaka 1964.

“Ninapenda kuwakaribisha wananchi wote wa Mkoa wa Mara na maeneo jirani kushuhudia kuwashwa kwa Mwenge wa Mwitongo kwa ajili ya kumuenzi Baba wa Taifa na Muasisi wa Mwenge wa Uhuru tarehe 18 Agosti, 2025 kuanzia saa sita mchana,” alisema.

Aidha, kiongozi huyo wa mkoa aliwaalika viongozi, watumishi wa serikali, taasisi binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi wote kushiriki Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 kwa kipindi chote utakapokuwa mkoani Mara.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025 ni Ismail Ali Ussi. Kaulimbiu ya mbio hizo inasema “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.”
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages