NEWS

Tuesday, 12 August 2025

Mbio za Urais 2025: Salum Mwalimu, mgombea mwenza wachukua fomu kuomba uteuzi INEC



Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele (wa pili kulia), akimkabidhi mteule wa CHAUMMA, Salim Mwalimu, mkoba wenye fomu za kuomba uteuzi wa kugombea urais katika ofisi za tume hiyo jijijini Dodoma leo.
---------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, ameongozana na mgombea mwenza wake, Devotha Minja, kuchukua fomu za kuomba uteuzi wa kugombea nafasi hiyo, katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma leo Agosti 12, 2025.

Mwenyekiti wa CHAUMMA Taifa, Hashim Rungwe, ni miongoni mwa viongozi na wanachama waliowasindikiza wagombea hao kuchukua fomu hizo.

Salum Mwalimu amesema ni furaha kubwa kwa yeye na chama chake hicho kuingia katika safari hiyo muhimu ya kisiasa ya kugombea urais, na kusisitiza kuwa hofu au vikwazo vyovyote vitakavyojitokeza haviweza kukwamisha azma yao ya kuleta mabadiliko makubwa kwa Watanzania.

“Tunakwenda kuibadilisha historia, kipaumbele chetu ni kuinua sauti ya wananchi na kuleta mageuzi, kampeni zetu rasmi tutazindua Zanzibar, ambapo tutaanza rasmi kuomba ridhaa kwa Watanzania wote kutuamini ili tuwatumikie,” amesema Mwalimu.

ameongeza: “Kama kiongozi msafi, sina deni lolote kwa mtu, sina aibu kwa sababu ya usafi wangu wa dhamiri na matendo, mimi na mgombea mwenza ni wasafi na tunatoa fikra safi, bila mawaa yoyote ambayo yangezuia mustakabali wa taifa letu.”

Kuhusu mabadiliko wanayotaka kuleta, Salum Mwalimu amefafanua kuwa msingi wa mageuzi yao utaanzia katiba. “Tutaenda kuanzisha serikali inayolenga haki za watu na kuwahakikishia uhuru wa kweli bila hiana yoyote,” amesema.

“Watanzania watarajie kuona Tanzania yenye neema na maendeleo ambayo Mungu ametupatia, tumekulia maisha ya umaskini lakini tunayaelewa maisha hayo na tunawapa matumaini Watanzania kuondokana na hali hiyo,” amesisitiza.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages