NEWS

Monday, 11 August 2025

Mbio za kinyang’anyiro cha Ikulu zashika kasi


Wateule wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi wakionesha mkoba wenye fomu za uteuzi wa kugombea Urais na Makamu wa Rais walizokabidhiwa na Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele (hayupo pichani), jijini Dodoma juzi.
---------------------------------------

Na Mwandishi Wetu

Mbio za Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilianza rasmi Jumamosi Agosti 9, 2025 baada ya mtetezi wa nafasi hiyo, Dkt. Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, kuchukua fomu za uteuzi kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa INEC, uchukuaji wa fomu za uteuzi kwa wagombea Urais na Makamu wa Rais umepangwa kufanyika Agosti 9 hadi 27, 2025 na kufuatiwa na utoaji wa fomu kwa wagombea ubunge na udiwani Agosti 14 hadi 27, 2025.

Uteuzi wa wagombea Urais na Makamu wa Rais, Ubunge na Udiwani utafanyika Agosti 27, 2025 kabla ya kuanza rasmi kwa kukurukakara za kampeni nchi nzima.

Dkt. Samia na mgombea mwenza, Dkt Nchimbi wanatetea Urais kwa tiketi ya chama tawala - CCM, ambacho ni moja ya vyama vikongwe barani Afrika, kikiwemo chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini.

Vyama vingine vilivyotangaza wagombea wa Urais na Makamu wa Rais kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao ni pamoja na ACT-Wazalendo na CHAUMMA.

Vingine ni Chama cha Wakulima (AAFP) kilichomweka Kunje Ngombale Mwiru na mgombea mwenza, Shum Juma Abdalla na NRA chenye mgombea urais, Hassan Kisabya Almas na mgombea mwenza, Ally Hassan.

Kwa upande wa chama cha MAKINI mgombea urais aliyependekezwa ni Coster Jimmy Kibonde na mgombea mwenza, Azza Haji Suleiman, NLD ikimemsimamisha Doyo Hassan Doyo na mgombea mwenza, Chausiku Khatibu Mohamed na UPDP ni Twalib Ibrahim Kadege.

Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele (kulia), akikabidhi fomu za uteuzi kwa Kunje Ngombale Mwiru, aliyependekezwa kugombea Urais kupitia AAFP, jijini Dodoma juzi. Kushoto ni mgombea mwenza, Shum Juma Abdalla.
----------------------------------------

ACT-Wazalendo kimemteua aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kisesa mkoani Simiyu kwa tiketi ya CCM, Luhaga Mpina, kuwa mgombea wake wa Urais.

Mpina hivi karibuni alijiondoa CCM baada ya kutoteuliwa kugombea ubunge baada ya kutumikia nafasi hiyo ya uwakilishi wa wananchi bungeni kwa miongo miwili.

Nacho CHAUMMA kimemteua Salum Mwalimu kugombea urais akiwa na mgombea mwenza, Devota Minja. Chama hicho kimepata nguvu baada ya kuwapokea wanachama waliohama kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, mgombea wa CCM, Dkt. Samia, atapambana na wagombea urais wapya ambao hawajawahi kushiriki katika chaguzi zilizopita chini ya mfumo wa vyama vingi ulioanzishwa nchini mwaka 1992.

Chama Cha Mapinduzi, ambacho kilizaliwa Februari 5, 1977 baada ya muungano wa vyama vya TANU (Tanzania Bara) na Afro-Shiraz Party (ASP) kwa upande wa Zanzibar, kinajivunia ukongwe wake na mtandao mkubwa wa wanachana nchi nzima ikilinganishwa na vyama vingine.

Mtandao wa CCM kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi taifa umekuwa ni mtaji mkubwa wa ushindi kwenye chaguzi mbalimbali zilizopita.

Ni kutokana na ukweli huo, ndiyo maana wachambuzi wa masuala ya siasa wanatabiri kwamba CCM itazoa kura nyingi za kuifanya iendelee kuunda serikali.

Miaka 30 tangu Tanzania iingie kwenye mfumo wa vyama vingi imeonesha kwamba upinzani umekuwa ukikosa mbinu madhubuti za kuikabili na kuishinda CCM ambayo imekuwa ikionekana kama "dude" lenye nguvu za kutisha.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema nguvu na uwezo wa upinzani kuweza kuhimili vishindo vya CCM vitaonekana bayana kipindi cha kampeni kwa nafasi zote - urais, ubunge na udiwani.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages