
Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza hafla ya kitaifa ya kuaga mwili wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri hiyo, Job Yustino Ndugai, katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo Agosti 10, 2025.
Ndugai ambaye siku chache zilizopita aliongoza katika kura za maoni za kutetea kiti cha Ubunge wa Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alifariki dunia Agosti 16, 2025 wakati akipatiwa matibabu jijini Dodoma baada ya kuugua kwa muda mfupi shinikizo la chini la damu lililosababishwa na maambukizi makali kwenye mfumo wa hewa.

Rais Samia akiwafariji wanafamilia ya Spika Mstaafu wa Bunge Job Yustino Ndugai katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo Agosti 10, 2025.

Akihutubia umati mkubwa waombolezaji katika hafla hiyo, Rais Samia alisema Ndugai alikuwa kiongozi mkomavu kisiasa na kiuongozi, ambaye aliweka thamani kubwa katika demokrasia ya Bunge.
“Ndugai alikuwa mkomavu kisiasa na kiuongozi, na aliyeamini katika demokrasia ya Bunge. Alipokuwa Spika, Bunge lilishuhudia mafanikio mbalimbali yaliyoelezwa hapa na Katibu wa Bunge,” amesema Rais Samia.
Wakati huo huo, kiongozi huyo wa nchi ameagiza mamlaka husika serikalini kujenga makumbusho yatakayoeleza mchango wa wilaya ya Kongwa katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika ili kuenzi ndoto ya Ndugai.
Hafla hiyo ya kuaga mwili wa Ndugai imehudhuriwa na viongozi wa kitaifa, wabunge, ndugu, jamaa na wananchi waliojitokeza kumuenzi marehemu huyo. Baadaye mwili wa Spika Mstaafu umesafirishwa kwenda Kongwa utakapozikwa.
No comments:
Post a Comment