NEWS

Tuesday, 12 August 2025

RC Mara aagiza kuwepo vikao vya kupata taarifa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri



Mkuu wa Mkoa wa Mara,
Kanali Evans Alfred Mtambi.
-------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, amemwagiza Katibu Tawala (RAS) wake kuanzisha vikao vya kila robo mwaka vya sekta za uzalishaji mali, biashara na maendeleo ya jamii kwa ajili ya kupata taarifa ya mikopo ya asilimia 10 iliyotolewa na halmashauri za mkoa huo.

Ameongeza kuwa taarifa hizo ziwe zinaambatana na kuonesha fursa zilizopo katika sekta mbalimbali ambazo wananchi wanaweza kuzichangamkia ili kujikwamua kiuchumi.

Kanali Mtambi alitoa maelekezo hayo wiki iliyopita ofisini kwake mjini Musoma, wakati alipoongoza kikao cha pili cha maandalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 katika Mkoa wa Mara na kusisitiza suala zima la maboresho ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu bila riba.

Aliwataka maafisa maendeleo ya jamii kuwa wabunifu katika utoaji wa mikopo hiyo ili kuongeza tija kwa vikundi husika.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa mkoa alishauri kutoelekeza nguvu kubwa ya mikopo hiyo kwa ajili ya biashara za kubeba abiria kwa kutumia pikipiki (bodaboda).

“Kuanzia sasa ninataka kuona mikopo inatolewa kwa vikundi ambavyo vitafanya biashara endelevu za uzalishaji mali, zenye tija na zinazoonesha ubunifu na siyo kila kikundi biashara ni ya bodaboda,” alisema Kanali Mtambi.

Aliwakumbusha maafisa maendeleo ya jamii jukumu la kuwahamasisha wananchi kubuni miradi yenye tija, endelevu na inayoweza kuboresha uchumi wao na halmashauri husika.

Kanali Mtambi alitoa mfano wa biashara za ufugaji wa samaki katika vizimba na kilimo cha umwagiliaji kulingana na mazingira ya maeneo wanayoishi.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages