
Na Christopher Gamaina
Mwaka huu wa 2025 una maana kubwa katika historia ya kisiasa ya Tanzania, ambapo taifa linakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29. Kampeni rasmi za uchaguzi huo zimeanza leo Agosti 28 na zitahitimishwa Oktoba 28, 2025.
Kipindi hiki ni fursa adhimu kwa vyama vya siasa na wagombea kuwasilisha ilani, sera, maono na mipango yao ya maendeleo ya kisekta kwa wananchi.
Hata hivyo, ni muhimu kuelewa kwamba hitaji la wananchi siyo tu sera za wanasiasa na vyama vya siasa, bali ni namna zinavyowasilishwa kwa amani, ustaarabu na kauli za staha.
Demokrasia siyo tu mchakato wa uchaguzi na kupiga kura, bali ni utamaduni wa kuheshimiana, kuvumiliana na kushindana kwa hoja. Hivyo, katika kipindi cha kampeni wanasiasa wanapaswa kuonesha mfano bora kwa jamii kwa kujikita katika kuelimisha umma kuhusu sera zao badala ya kushambuliana kwa matusi, kejeli au vitisho.
Kauli chafu, lugha za uchochezi na fujo siyo tu zinavunja maadili ya kisiasa, bali pia zinatishia amani, upendo na mshikamano wa kitaifa uliojengwa kwa miongo kadhaa.
Tanzania imejijengea sifa ya kuwa kisiwa cha amani katika bara la Afrika. Amani hii haikuja kwa bahati; ni matokeo ya juhudi za pamoja za wananchi, viongozi na taasisi mbalimbali za kitaifa.
Katika kipindi cha kampeni, ni wajibu wa kila mwanasiasa na chama cha siasa kuhakikisha kuwa kauli wanazotumia haziibui chuki, hofu wala migawanyiko ya kijamii, kisiasa au kidini.
Tunapaswa kukumbuka kuwa baada ya uchaguzi, maisha yataendelea, Watanzania wote tutaendelea kuishi pamoja kama ndugu wa taifa moja.
Kwa upande mwingine, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vina mchango mkubwa katika kueneza taarifa za kampeni. Hata hivyo, kuna haja ya kutumia majukwaa haya kwa umakini mkubwa.
Vyombo vya habari vinapaswa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari kwa kutoa habari sahihi, zisizopendelea upande wowote na zinazochochea mjadala wa kimaendeleo.
Vilevile, watumiaji wa mitandao ya kijamii wanapaswa kuepuka kusambaza taarifa za uongo, chuki au matusi dhidi ya wagombea au wafuasi wa vyama vingine.
Kwa viongozi wa vyama vya siasa, kampeni ni muda wa kuonesha dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi. Ni kipindi cha kutangaza sera zinazogusa maisha ya watu, si muda wa kutafuta umaarufu kwa kubeza wengine.
Tunawaomba viongozi wote kuhakikisha wanawafundisha wafuasi wao maadili ya siasa safi – kutokujibu kwa jazba, kutovuruga mikutano ya wapinzani na kuzingatia kuhubiri amani na utulivu katika kila jukwaa la kampeni watakalokanyaga.
Uchaguzi Mkuu wa 2025 ni fursa ya kuimarisha misingi ya demokrasia ya Tanzania. Ni muda wa kuthibitisha kuwa taifa letu linaweza kushindana kisiasa bila kuvuruga amani na mshikamano wa kitaifa.
Kwa kuzingatia kampeni za amani, zenye hoja zenye mashiko na kauli za staha, tutajenga taifa lenye heshima, mshikamano na mustakabali bora kwa kizazi cha sasa na vijavyo. Tuikumbuke siasa ni ushindani wa hoja na sera, si chuki na uhasama wa mioyo.
No comments:
Post a Comment