
Na Godfrey Marwa, Tarime
Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) mkoani Mara imeadhimisha Juma la Elimu, ambapo imeelimisha jamii umuhimu wa elimu ya msingi na sekondari kwa watoto wa kike na kiume.
Maadhimisho hayo yalifanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Nyamongo katani Matongo jana Septemba 3, 2025, ambapo halmashauri ilitumia nafasi hiyo pia kutangaza fursa ya elimu msingi na sekondari bure kwa walioikosa kwa njia mbadala kuanzia Januari 2026 ili waweze kutimiza ndoto zao.

Walengwa wa fursa hiyo ya elimu bila malipo ni pamoja na walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo maradhi au ugonjwa, ujauzito, hali duni ya maisha, migogoro ya kifamilia, utoro na kuhamahama.
Shule ya Sekondari Nyamongo ndiyo imeteuliwa kuwa kituo kitakachoanza kutoa elimu hiyo ya bila malipo, ambapo wa sekondari watasoma kidato cha kwanza hadi cha nne kwa miaka miwili.
Kwa upande wa wanafunzi wa elimu ya msingi wenye mahitaji maalum kutakuwa na vituo viwili ambavyo ni Shule ya Msingi Kwihore iliyopo kata ya Matongo na Shule ya Msingi Mwema iliyopo kata ya Mwema.


Maadhimisho hayoya yalihudhuriwa na wazazi, walimu na wanafunzi wa shule zote za msingi na sekondari zilizopo kata ya Matongo eneo la Nyamongo, ambapo walishiriki kwa kuonesha vipaji vya kuigiza na kusoma ushairi.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Afisa Elimu ya Watu Wazima Idara ya Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Marina Atupele Ngailo.

"Tumeamua kuleta maadhimisho haya hapa Nyamongo ili kuleta chachu kwa wanafunzi, wazazi na wadau wa elimu kuhamasisha watoto walioacha shule kurudi shuleni. Serikali chini ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan imeleta programu mbalimbali kusaidia watoto walio nje ya mfumo rasmi kupata elimu.
"Kwa shule ya msingi kuna programu inayoitwa MEMKWA, SEKWIPU kwa sekondari na MKEJA - Mpango wa Uwiano kwa Jamii ambao unawasaidia wale ambao hawakuweza kupata elimu wakiwa na umri mdogo, watafundishwa mambo ya ujasiriamali, mfano kutengeneza sabuni, batiki na vitu mbalimbali.
"Ninyi wanafunzi tunawasihi mkawahamasishe watoto wenzenu warudi shuleni bila kuwaacha ndugu zetu wenye mahitaji maalum," alisema Ngailo.

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nyabichune, Vaileti Ezekiel, akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema: "Hii siku tumeweza kujifunza mambo mengi ambayo yanatujenga kimwli na kielimu, tumejifunza wanafunzi walioacha shule kwa kupitia mambo magumu, mfano ujauzito, kuhama, ugumu wa maisha tuweze kuwashawishi waje kwenye vituo wasome bure na kufikia malengo yao."
Pia, maadhimisho hayo ya Juma la Elimu yalifanyika sambamba na ukaguzi wa zana za kufundishia wanafunzi wa sekondari na msingi, hasa MEMKWA pamoja na maonesho ya wajasiriamali wa bidhaa mbalimbali.

No comments:
Post a Comment