NEWS

Monday, 1 September 2025

Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Serikali wajenga stendi ya kisasa Nyang’hwale



Magari ya abiria yakiwa katika sehemu ya stendi mpya ya Ikangala, Nyang’hwale iliyojengwa kutokana na fedha za CSR Barrick Bulyanhulu.
------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Nyang’whale

Mgodi wa Dhahabu wa Barrick Bulyanhulu kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, mkoani Geita umejenga stendi ya kisasa ya Ikangala kwa gharama ya shilingi milioni 299.9.

Hatua hiyo imewaondolea wananchi kero ya muda mrefu ya kutokuwepo stendi ya mabasi katika halmashauri hiyo.

Hafla ya uzinduzi wa stendi hiyo ilifanyika wiki iliyopita na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wananchi na wafanyakazi wa Barrick, mgeni akiwa Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame.

Katika hotuba yake, Kingalame alisema miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na wawekezaji ni matunda ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini.

Aliwataka wananchi, wafanyabiashara na wadau wote wa usafirishaji kutumia fursa ya stendi hiyo katika kujikwamua kiuchumi.

“Natoa rai kwa wananchi na wadau wote wa usafirishaji waweze kutumia fursa ya uwepo wa stendi hii kujikwamua kichumi kupitia biashara mbalimbali zinazotokana na mahitaji ya utoaji wa huduma kwa wasafiri," alisema Kingalame.


Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa stendi hiyo.
-------------------------------------------

Awali, Meneja wa mradi huo, Mhandisi Bruno Marco, alisema ujenzi huo unatekelezwa kwa awamu kwa kutumia mfumo wa mkandarasi kwa baadhi ya kazi na wataalamu wa ndani (Force Akaunti), na kwamba hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 85.

“Ujenzi wa Stendi ya Ikangala unajumuisha miundombinu mbalimbali, ikiwemo choo, eneo la kuegesha magari ya abiria, majengo ya abiria, huduma ya chakula, mkusanya mapato, polisi, kizimba cha kuhifadhia taka, fremu za maduka,” Marco alifafanua.

Mwakilishi wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu, David Magege, ambaye ni Afisa Uhusiano wa Jamii katika mgodi huo, aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa mradi huo na miradi mingine inayoendelea kutokana na fedha za CSR.

Magege aliihamasisha Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) katika eneo hilo kuendelea kuibua miradi yenye tija inayolenga kuleta maendeleo na kunufaisha wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Wafanyabishara Wadogo (Machinga) wa wilaya hiyo, Dorcas Hussein, alisema stendi hiyo itawapatia fursa ya kujiendeleza kibiashara na kujikwamua kiuchumi. “Tunashukuru Serikali na Barrick Bulyanhulu kwa kuendelea kutuletea miradi ya maendeleo," alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages