NEWS

Sunday, 28 September 2025

Mwanza Precious Metals yakusanya zaidi ya tani tano za dhahabu kwa niaba ya BoT




Na Mwandishi Wetu
Mwanza
--------------

Zaidi ya tani tano za dhahabu zimekusanywa na kusafishwa na kiwanda cha Mwanza Precious Metals Refinery ambacho hufanya kazi hiyo kwa niaba ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Nyaisara Mgaya, aliyoitoa wiki hii kwa ujumbe wa nchi jirani ya Malawi ambao ulitembelea Mwanza kwa mafunzo ya usimamizi na uendeshaji wa biashara ya madini, hususan mfumo wa masoko unaotumika Tanzania.

Kiwanda cha Mwanza Precious Metals Refinery kina uwezo wa kusafisha kilo 960 za dhahabu kwa siku lakini kutokana na ukosefu wa upatikanaji wa malighafi hivi sasa kina uwezo wa kusafisha kilo 480 kwa siku, Mhandisi Mgaya aliiueleza ujumbe wa Malawi.

Tanzania ni nchi iliyopiga hatua katika usimamizi madhubuti wa rasilimali madini, jambo ambalo limeyavuta baadhi ya mataifa Afrika kuja kujifunza uendeshaji wake.


Mhandisi Nyaisara Mgaya

Kiongozi wa ujumbe wa Malawi ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara za Vikundi, Zizwan Khonje, aliisifu Tanzania kwa kuwa na mfumo imara wa biashara na masoko ya madini.

“Tanzania ni mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na hatua mbalimbali ilizochukua kuboresha sekta ya madini, ikiwemo uanzishaji wa masoko ya madini ya wazi na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa rasilimali hizi,” alisema.



Ujumbe wa Malawi pia ulipata nafasi ya kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, na kuonana na Katibu Tawala wa mkoa huo, Balandya Elkana.



Ziara ya ujumbe wa Malawi itakuwa kichocheo kwa nchi hiyo kufanya mageuzi katika sekta yake ya madini kwa kuimarisha mifumo ya usimamizi kuhakikisha kwamba mapato ya serikali yanaongezeka na wachimbaji wadogo wanawezeshwa na kushirikishwa kikamilifu ili kukuza uchumi wa taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages