NEWS

Monday, 8 September 2025

Ndege za kitanzania zinazoruka kwa mafuta ya bodaboda



Moja ya ndege tisa zinazoundwa sasa katika Karakana ya uwanja wa Mazimbu, mkoani Morogoro. Tano zimekamilika na kutumika.

Yusuph Mazimu
Akiripoti kutoka
BBC Dar es Salaam
----------------------------

Katika uwanja mdogo wa ndege wa Mazimbu, Morogoro, nilijikuta nikishuhudia jambo ambalo kwa wengi lingesikika kama hadithi tu. Hapa, kundi la vijana 13 wa Kitanzania wanapiga hatua kubwa kwa kutengeneza ndege ndogo kwa mikono yao hatua moja kubwa kuelekea historia mpya ya anga barani Afrika.

Nilipoingia ndani ya Karakana yao ndogo, nilikumbwa na sauti za mashine zikikata chuma, vijana wakikaza skrubu na wengine wakipima mabawa ya ndege kwa umakini. Nilihisi kama nimeingia kwenye ulimwengu wa kipekee usiotarajiwa kuwa katikati ya Morogoro.

Hapa wanaunda ndege ndogo aina ya Sky leader 500 na Sky leader 600 zenye injini moja na uwezo wa kubeba abiria wawili. Zina kasi ya hadi kilomita 265 kwa saa, umbali wa safari wa kilomita 1,600 kwa tanki moja, na matumizi ya petroli ya kawaida lita 120 pekee. Kinachoshangaza zaidi, zinaweza kutua kwa kutumia njia fupi ya mita 100 pekee hata kwenye majani.

Paul Ihuya, kijana aliyekuwa wa kwanza kuanza safari hii, ananieleza akionekana bado ana shauku na msisimko mkubwa: "Furaha niliyokuwa nayo siku naiona ndege niliyoitengeneza kwa mikono yangu na imeruka salama, haiwezi kuelezeka."

Usalama na ubora kipaumbele chao kikubwa

Nilipata nafasi ya kuruka na ndege hii kwa wastani wa nusu saa katika anga ya Morogoro chini ya rubani Mtanzania Engelbert Sengati (kulia).

Swali ambalo wengi huuliza ni: "Je, ndege hizi ni salama kweli?" Injinia Lilian Jackson, fundi anayehakikisha ubora, anakazia kwamba kila kitu kimefuata taratibu za kimataifa. "Ndege ndicho chombo kinachoamini kwa asilimia 100 kwa usalama, kwa hiyo tunahakikisha ndege zetu ziko kwenye ubora unaotakiwa ili kuhakikisha usalama na kuepusha ajali," anasema Lilian.

Mara yangu ya kwanza kuipanda ndege hii nilihisi hofu. Ndani ina viti vizuri, sehemu ya miguu unainyoosha vyema, inafunguka kwa juu kukiwa na kioo ambacho kinakupa nafasi ya kuona vizuri mandhari ya angani. Nilikaa ndani nikitazama rubani Engelbert Sengati akijiandaa kwa safari ya kunizungusha kwenye anga ya Morogoro. Alinipa miongozo ya usalama kama ilivyo kawaida.

Mara ya kwanza tuliporuka na kuzunguka juu kwa nusu saa, nikihisi mwili wangu wote unahofu. Sio rahisi. Lakini kadri muda ulivyoendelea, niliona tofauti ni ndogo sana na ndege ndogo nyingine nilizowahi kupanda. Imetulia, salama, na inatii kila amri ya rubani.

Nikatua na kwenda raundi ya pili. Safari hii nilijikuta mdadisi zaidi… nikaanza kupiga picha, kuzungumza na rubani, na kumuuliza maswali mengi. Alinihakikishia kuwa ndege hizi zimetathminiwa na mamlaka na zimethibitishwa kwa ubora na usalama.

Hapo hofu yangu ikayeyuka kabisa ikibaki hisia moja kuu ya uzalendo. Nilijisemea moyoni: "Wooo… hii ni ndege ya Watanzania. Imetengenezwa na vijana wetu hapa Tanzania. Imetengenezwa Afrika." Kwakweli hisia ya fahari ilinijia, fahari ya kuwa Mtanzania, na zaidi, fahari ya kuwa Mwafrika.


Injinia Lilian Jackson

"Sikuamini watanzania wanaweza kutengeneza ndege."

Kwa wakazi wa kawaida, ndoto hii bado inashangaza. Said John, mwenyeji wa Tanga, anakiri: "Mimi nilipata mshtuko kidogo kwamba Watanzania wanaweza kuunda ndege kwa mikono yao. Kwanza sikuamini. Nilidhani wanaletewa vifaa wanaviunganisha tu. Lakini baada ya kuona kwenye video nikaamini na nikaona sasa tumefika pazuri."

Lakini bado kuna wanaobaki na mashaka. Safi Ruda, wa Dar es Salaam, anasema kwa mshangao: "Watanzania kutengeneza ndege? Ndege hizi hizi zinazopaa juu? Hapana, ni kitu ambacho siamini."

Kwa maneno haya, unapata taswira ya safari ilivyo. Ni hadithi inayobeba mshangao, shaka, lakini pia matumaini na fahari mpya.

Tanzania kitovu cha uzalishaji wa ndege Afrika

Vijana wakiendelea na uzalishaji wa ndege kuanzia hatua ya kwanza.

Tayari vijana hawa ambao mbali na kupata mafunzo nchini walipata nafasi ya kwenda Czech Republic kwa muda mfupi kujifunza kwa vitendo utengenezaji wa ndege tayari wameunda ndege 9, na tano kati ya hizo zinatumika kikamilifu.

Wanasema kama wana kila kitu wanauwezo wa kuunda ndege moja kila mwezi kupitia kampuni yao ndogo, Airplanes Africa. Paul Ihuya anafafanua malengo yao ya baadaye: "Tunataka kwenda mbali zaidi. Hatutaki tu kujulikana kwa ndege ndogo. Lengo letu ni kuunda hata ndege kubwa za abiria na kuthibitisha kuwa Tanzania inaweza kuwa kitovu cha anga Afrika."

Kwa dunia inayozidi kuzungumza juu ya nafasi ya vijana na ubunifu barani Afrika, hadithi hii ya Mazimbu inatoa picha ya kile kinachowezekana.

Kwa hakika Mazimbu, Morogoro unaweza kusema hapa ndipo ndoto za vijana hawa 13 zinapaa angani. Hii siyo tu hadithi ya ndege, bali ni hadithi ya kizazi kipya kinachoamini kuwa hakuna kisichowezekana. Ujuzi wa anga mpya unazaliwa huku safari ya ndoto ndiyo kwanza inaanza.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages