
Mkurugenzi wa Professor Mwera Foundation, Hezbon Peter Mwera.
NA MWANDISHI WETU, Tarime
------------------------------------------
TAASISI ya Professor Mwera (PMF) imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuwa chachu ya maendeleo ya elimu kwa watoto wa Kitanzania, baada ya kutangaza ofa maalum ya kuwalipia wanafunzi 12 waliohitimu darasa la saba katika Shule ya Msingi Mwera Vision mwaka huu ada za masomo ya sekondari.
Watasoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule binafsi ya Sekondari Tarime Mchanganyiko, huku pia kila mmoja akipewa fursa ya kusoma kozi ya ufundi anayopenda katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime, vinavyomilikiwa na taasisi hiyo katika mji wa Tarime, mkoani Mara.
Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera, alitangaza ofa hiyo wakati wa Mahafali ya Tano ya Darasa la Saba ya shule hiyo - yaliyofanyika shuleni hapo Agosti 28, 2025 akisema hatua hiyo ni sehemu ya dhamira endelevu ya taasisi hiyo katika kuwapunguzia wazazi na walezi mzigo wa gharama za masomo kwa watoto wao, ikiamini kuwa elimu ni urithi bora kuliko mali yoyote.

Kupitia ofa hiyo, wanafunzi wote 12 (wavulana sita na wasichana sita) watanufaika moja kwa moja, ambapo PMF itamlipia kila mmoja ada ya shilingi milioni 1.5 kwa mwaka, sawa na shilingi milioni 18 kwa mwaka kwa wanafunzi wote 12.
Hivyo, jumla ya gharama itakayobebwa na taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka minne ya elimu ya sekondari na kozi za ufundi kwa wanafunzi hao ni shilingi milioni 72.
Mkurugenzi Hezbon alisisitiza kuwa elimu ni njia ya kujikomboa na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa jamii nzima, na kwamba PMF haitazami elimu kama huduma ya kibiashara, bali kama haki ya msingi kwa kila mtoto.
PMF inaamini kuwa kupitia uwekezaji huo, itasaidia kuibua kizazi chenye maarifa, stadi na maadili, kitakachojenga Taifa lenye ushindani na ustawi.
"Taasisi ya Professor Mwera itakwenda kusimamia karo ya wanafunzi wote pamoja na kozi moja ya ufundi bure kuwaunga mkono wazazi waliosomesha wanafunzi hapa kuanzia chekechea mpaka la saba," alisema Hezbon.
Mkurugenzi huyo wa PMF alitumia nafasi hiyo pia kuwakaribisha wazazi na walezi kupeleka watoto wao kusoma katika shule hizo kwa gharama nafuu.
"Sisi tunajivunia utofauti tulionao, gharama kwetu ni nafuu sana, tunaamini kuwa hatujafika hapa bila kushikwa mkono, hatuangalii kutengeneza faida. Ukiwa mbinafsi Mungu anakunyang’anya ulichonacho - ndio maana unaona tunatoa ofa, ikiwemo ya kusomesha vijana wa Tarime bure. Mpaka sasa tumeishasomesha vijana zaidi ya elfu sita," alieleza.
Hatua ya PMF kutangaza ofa ya kuwalipia ada wanafunzi hao 12 imepokewa kwa furaha na matumaini makubwa kutoka kwa wazazi, walezi na wanafunzi hao, wakieleza kuwa msaada huo ni mkombozi mkubwa katika kipindi hiki ambapo watu wengi wanakumbwa na changamoto za kiuchumi.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mwalimu Revocatus Baru, aliahidi kuipatia shule hiyo msaada wa kompyuta, huku akihimiza umuhimu wa elimu ya ufundi kwa vitendo.
"Sasa tunataka watoto wanaomaliza shule ya msingi watoke na fani ya ufundi ili iwasidie maishani - hata asipoendelea na masomo,” alisema Mwalimu Baru.
Alimpongeza Mkurugenzi wa PMF, Hezbon, kwa ubunifu katika shule hiyo na kumwahidi makubwa. “Shule hii tunaenda kuiboresha, tuko tayari kusaidia vitabu vya mtaala mpya. Wazazi tusikose kuleta wanafunzi kwenye shule hizi zenye mkondo wa amali," alisema.
Nao wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwera Vision, akiwemo Grace Michael, waliahidi kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya kitaifa ili kupata matokeo mazuri - wakisema wamefundishwa kwa weledi wa hali ya juu kukuza vipaji vyao na kulelewa kiroho.
Mahafali hayo pia yalipambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi, pamoja na ushuhuda wa baadhi ya wazazi kuhusu mchango wa shule ya Mwera Vision katika kulea watoto wao kitaaluma, kinidhamu na kiroho.
Ilikuwa ni siku ambayo jamii ilijifunza kuwa ndoto za watoto wa kawaida zinaweza kutimia – endapo tu kutakuwa na watu walio na moyo wa kusaidia kama Taasisi ya Professor Mwera.
Kwa ujumla, uamuzi wa taasisi hiyo wa kutoa ofa hiyo umesifiwa kama mfano wa kuigwa, unaoonesha mshikamano kati ya sekta binafsi na jamii katika kukuza elimu ya msingi, sekondari na ufundi kwa watoto na vijana wa Kitanzania.
No comments:
Post a Comment