
Na Mwandishi Wetu
Serengeti
-------------

Serengeti
-------------
Taasisi ya Nyansaho (Nyansaho Foundation) imekabidhi msaada wa mabasi mapya matatu kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ambaye naye ameyakabidhi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa ajili ya shule za sekondari Machochwe, Ngoreme na Natta za wilayani Serengeti.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika mjini Mugumu leo Septemba 30, 2025, ambapo imehudhuriwa na Mwasisi na Mwenyekiti wa Nyansaho Foundation, Dkt. Rhimo Nyansaho, viongozi wengine wa serikali, wazazi, walimu, wanafunzi na wananchi mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa ya Nyansaho Foundation, ununuzi wa mabasi hayo umeigharimu taasisi hiyo shilingi zaidi ya milioni 300.
Mabasi hayo yanatarajiwa kuwapunguzia kama si kuwaondolea wanafunzi wa shule hizo adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za elimu, hali iliyokuwa ikiathiri mahudhurio na ufaulu katika shule hizo.
Dkt. Nyansaho amesema lengo ni kuziwezesha shule hizo zilizoko pembezoni mwa wilaya kupata usafiri wake, na kwamba licha ya kununua mabasi hayo yamepewa usajili wa serikali ikiwemo bima.
“Nilipoalikwa kwenye mahafali ya shule za sekondari Machochwe na Ngorome walisema changamoto ya magari, nami nikaahidi, kule Natta High School wao hawakuomba kutokana na misaada mingi tuliyokuwa tumetoa, lakini niliona kuna haja wapate usafiri.
“Niliamua Natta nao wapate ili iwe inasaidia shule zilizoko ukanda huo kama Makundusi, Robanda, Nagusi na Rigicha, tunaomba matumizi yake yawe mazuri ili kutatua changamoto za usafiri kwa shule zetu,”amesema Dkt. Nyansaho.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (kulia), akipokewa mabasi mapya matatu kutoka kwa Nyansaho Foundation. Katikoti ni Mwasisi na Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Dkt. Rhimo Nyansaho.
RC Mtambi amemshukuru na kumpongeza Dkt. Nyansaho kwa moyo wa uzalendo uliooneshwa, akisema msaada huo ni ushahidi wa dhati wa namna sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na serikali katika kuboresha huduma za kijamii.
Amesema msaada huo ni sehemu ya mpango mpana wa taasisi hiyo wa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha elimu mkoani Mara.
Ameongeza kuwa jitihada za Nyansaho Foundation katika kusaidia maendeleo ya jamii zimekuwa zikionekana, na kwamba hadi sasa mchango wake kwa maendeleo ya m,koa wa Mara umefikia shilingi zaidi ya bilioni nne.
Nao wanafunzi, walimu na wazazi wameishukuru Nyansaho Foundation wakisema msaada huo wa mabasi utaleta mapinduzi makubwa katika mazingira ya elimu.
Nyansaho Foundation imejizolea sifa kwa uwekezaji wake mkubwa kwenye sekta za elimu na afya, miongoni mwa myingine mkoani Mara.
No comments:
Post a Comment