NEWS

Wednesday, 1 October 2025

Ujumbe wa Malawi wavutiwa na usimamizi thabiti wa sekta ya madini Tanzania




Na Mwandishi Wetu
Mwanza
---------------

Ujumbe wa Serikali ya Malawi ambao mwishoni mwa wiki iliyopita ulikuwa Tanzania kwa ziara ya kikazi umeonesha kuvutiwa na usimamizi thabiti na mfumo wa uendeshaji wa sekta ya madini.

Ujumbe huo ulioongozwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara za Vikundi, Zizwan Khonje, uliisifu Tanzania kwa kuwa na mfumo imara wa biashara na masoko ya madini.

Katika ziara yake mkoani Mwanza, ujumbe huo ulitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kufanya mazungumzo na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Balandya Elkana, kisha kutembelea kiwanda cha kusafisha madini cha Mwanza Precious Metals Refinery.

Ukiwa kwenye kiwanda hicho, ujumbe huo ulielezwa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa, Mhandisi Nyaisara Mgaya, kwamba zaidi ya tani 65 za dhahabu zilikusanyawa na kusafishwa kwa niaba ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kiwanda cha Mwanza Precious Metals Refinery kina uwezo wa kusafisha kilo 960 za dhahabu kwa siku lakini kutokana na ukosefu wa upatikanaji wa malighafi hivi sasa kinasafisha kilo 480 kwa siku, Mgaya aliueleza ujumbe wa Malawi.

Tanzania ni nchi iliyopiga hatua katika usimamizi madhubuti wa rasilimali madini, jambo ambalo limeyavuta baadhi ya mataifa Afrika kuja kujifunza uendeshaji wake.

“Tanzania ni mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na hatua mbalimbali ilizochukua kuboresha sekta ya madini, ikiwemo uanzishaji wa masoko ya madini ya wazi na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa rasilimali hizi,” alisema Khonje, kiongozi wa msafara wa ujumbe wa Malawi.

Ziara ya ujumbe wa Malawi itakuwa kichocheo kwa nchi hiyo kufanya mageuzi katika sekta yake ya madini kwa kuimarisha mifumo ya usimamizi, kuhakikisha kwamba mapato ya serikali yanaongezeka na wachimbaji wadogo wanawezeshwa na kushirikishwa kikamilifu ili kukuza uchumi wa taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages