NEWS

Tuesday, 9 September 2025

Prof. Muhongo: CCM Musoma Vijijini hatuna upinzani kwenye kata 11



Prof. Sospeter Muhongo akisaka kura katika moja ya mikutano yake ya kampeni Musoma Vijijini wiki iliyopita.

NA MWANDISHI WETU, Musoma
---------------------------------------------

MGOMBEA wa ubunge jimbo la Musoma Vijijini kupitia CCM, Prof. Sospeter Muhongo, amesema wagombea wa chama hicho wa nafasi ya udiwani hawana wapinzani katika kata 11.

Hivyo, kinachosubiriwa ni wagombea wa kata hizo kupigiwa kura za ndiyo katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini Oktoba 29, 2025.

“Kata 11 hatuna mpinzani, tunapambana kwenye kata 10 ili tupate ushindi wa kura nyingi kwenye kata hizo zote,” Prof. Muhongo alisema katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake Musoma Vijijini wiki iliyopita.

Prof. Muhongo aliwaomba wakazi wa jimbo hilo kuwachagua wagombea wa CCM wa nafasi za urais, ubunge na udiwani akisema chama hicho kimefanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo afya na mindombinu ya barabara chini ya Rais Dkt. Samia Suhulu Hassan.

Alitolea mfano wa barabara ya lami ambayo imeanza kujengwa katika jimbo hilo ya Musoma- Busekera akisema ujenzi wake utaendelezwa kwa kasi mara baada ya Uchaguzi Mkuu.

“Barabara yetu ya lami tumeishajenga kilomita tano, tumeshaiwekea taa, serikali imeishampata mkandarasi. Kama tunataka barabara ya lami kutoka Musoma- Makojo- Busekera lazima tuichague CCM, lazima tumchague Mama Samia na Nchimbi, ni busara mnichague mimi,” alisisitiza wakati akihutubia mkutano mkubwa wa kampeni.

Prof. Mugongo aliongeza kuwa Serikali ya CCM pia imejenga hospitali na vituo vya afya vya kisasa Musoma Vijijini, na kwamba tayari ameiomba ujenzi wa vituo vya afya vingine vitano ili kuboresha zaidi huduma za afya katika jimbo hilo.

“Kituo cha afya kipya kinachojengwa kitafanya idadi ya vituo vya afya katika jimbo letu kuwa saba na nimeomba vingine vitano. Sasa hamuwezi kumpatia urais mtu mwingine ambaye sijampatia maombi yangu. Ni lazima tumchague Rais Samia kwa kura nyingi,” alisisitiza Prof. Muhongo.

Mgombea huyo pia alitangaza kuwa miaka mitano ijayo itakuwa ya mageuzi makubwa ya kiuchumi katika jimbo hillo, na kwamba juhudi kubwa zitaelekezwa kwenye uvuvi wa kutumia vizimba katika Ziwa Victoria na ujenzi wa kiwanda cha minofu ya samaki.

Prof. Muhongo anatajwa kama mmoja wa wabunge wanaokubalika zaidi kwa wananchi katika mkoa wa Mara kutokana na ubunifu wake na juhudi kubwa anzaofanya kuwaletea wananchi wa Musoma Vijijini maendeleo ya kisekta.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages