
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Dkt. Maulid Suleiman Madeni (kulia), akimshukuru Meneja wa Four Seasons Safari, Ahmed Attas.
NA MWANDISHI WETU, Serengeti
---------------------------------------------

---------------------------------------------
SHULE ya Sekondari Robanda iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara imepokea msaada wa vitanda 40, magodoro 80 na taa nane kutoka Kampuni ya Four Seasons Safari.
Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo shuleni hapo wiki iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Dkt. Maulid Suleiman Madeni, aliishukuru kampuni hiyo akisema vitakuwa chachu ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza hamasa kwa wanafunzi, hasa wanaoishi shuleni hapo.
"Mchango huu wa Four Seasons si tu kwamba umepunguza mzigo kwa serikali, bali pia umewapa faraja wanafunzi wetu ambao walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya uhaba wa vitanda na magodoro, na hii itaongeza hamasa kwao kusoma kwa bidii," alisema na kuwataka viongozi na wanafunzi wa shule hiyo kutunza vizuri vifaa hivyo ili vidumu muda mrefu.

Dkt. Madeni alitumia nafasi hiyo kuwaomba wadau wengine, zikiwemo kampuni zinazofanya kazi ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kuiga mfano wa Four Seasons Safari kwa kuchangia katika miradi mbalimbali ya maendeleo, hasa kwenye sekta za elimu, afya na maji, ambazo ndio nguzo kuu za maisha ya wananchi.
Kwa upande wake Meneja wa Four Seasons Safari, Ahmed Attas, aliushukuru uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa kuendeleza ushirikiano wa serikali na kampuni hiyo, huku akiahidi kuendelea kushiriki kikamilifu katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Nao wanafunzi wa shule hiyo, walieleza furaha yao baada ya kupokea vitanda, magodoro na taa wakisema kupitia msaada huo wataongeza bidii katika kusoma, kwani mazingira ya shule yao yanizidi kuboreshwa, ambapo waliahidi kufanya vizuri katika mtihani yao ili wazidi kuitia moyo serikali na wadau wengine wa maendeleo.
No comments:
Post a Comment