NEWS

Tuesday, 16 September 2025

RC Mtambi ataka jitihada zaidi kuimarisha ulinzi, uhifadhi wa Mto Mara




Na Mwandishi Wetu, Butiama

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amehimiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa Bonde la Mto Mara kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Kanali Mtambi alisisitiza hayo jana Septemba 15, 2025 kwenye hotuba yake ya kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya 14 ya Siku ya Mto Mara yaliyofanyika sambamba na maonesho ya ujasiriamali na upandaji wa miti wilayani Butiama, mkoani humo.

"Maadhimisho haya yamefanyika kwa viwango vikubwa, nawapongeza wananchi na wadau wote, sisi ni mashahidi kuwa Mto Mara una umhimu mkubwa katika kuchangia maendeleo endelevu,” alisema na kuendelea:

“Mto huu umezifanya mbuga zote mbili; Serengeti na Masai-Mara kuwa moja ya maajabu saba ya urithi wa dunia na pia ni muhimu kwa malisho na uzazi kwa wanyama hao [wanyamapori].”

Aliongeza: "Kupitia maadhimisho haya, natoa wito kwa wananchi kuhifadhi mazingira na kuhakikisha ikolojia ya Mto Mara inalindwa kwa ajili ya maisha yetu. Maadhimisho ni njia ya kudumisha umoja wetu, tunalo jukumu la kuhakikisha uhifadhi wa Bonde la Mto Mara unakuwa endelevu.”

"Bonde linakabiliwa na shughuli za kilimo, uchimbaji na ufugaji, kutokana na changamoto hizo, serikali kupitia Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria inaendelea kuchukuwa hatua. Nitoe rai kwa wananchi kutofanya shughuli zinazoathiri ikolojia na baioanuai ya Bonde la Mto Mara,” alisema Kanali Mtambi.

Alisisitiza kuwa ili kuimarisha uhifadhi wa Bonde la Mto Mara, kuna haja na ulazima wa kufanya jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kuendeleza Mto Mara.

Alihimiza nchi wanachama (Tanzania na Kenya) kuendelea kutekeleza mikataba ya usimamizi na uendelezaji wa Bonde la Mto Mara, ikiwemo kukamilisha mpango wa pamoja wa matumizi bora ya maji na kampeni ya kupanda miti rafiki kwa maji katika bonde la hilo.

Maadhimisho hayo ya Siku ya Mto Mara yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, mawaziri waandamizi wa nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki na wananchi wa mkoani Mara.

Wizara ya Maji na Mgodi wa Barrick North Mara walitunukiwa vyeti vya kutambua michango yao katika kufanikisha maadhimisho hayo pamoja na jtihada za kuhifadhi vyanzo vya maji.


Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandishi Mwajuma waziri (wa pili kulia), akipokea kutoka kwa RC Mtambi kikombe na cheti kutambua mchango wa wizara hiyo katika uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Mwakilishi wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara (wa pili kulia) akipokea cheti cha shukrani kwa kuwa miongoni mwa wadau walichangia kufanikisha maadhimisho hayo ya Siku ya Mto Mara.

Tanzania na Kenya zimekuwa zikiadhimisha Siku ya Mto Mara Septemba 15 kila mwaka kwa kupokezana, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza juhudi za pamoja za uhifadhi endelevu wa Bonde la Mto Mara unaotiririsha maji katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

Kwa kutambua umuhimu wa ikolojia ya Mto Mara, kikao cha 10 cha Sekretarieti ya Mawaziri wa Bonde la Ziwa Victoria kilichofanyika Kigali nchini Rwanda Mei 4, 2012 kiliazimia Septemba 15 kila mwaka kuwa Siku ya Mto Mara.

Maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Mto Mara yalifanyika mwaka 2012 nchini Kenya na kwa upande wa Tanzania maadhimisho ya kwanza ya siku hiyo yalifanyika mwaka 2013 katika mji wa Mugumu, wilayani Serengeti.

Mbali na umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori, inakadiriwa kuwa maisha ya watu zaidi ya milioni moja hutegemea uwepo wa Bonde la Mto Mara upande wa Tanzania na Kenya.

Aidha, watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani wamekuwa wakimiminika kushuhudia makundi ya nyumbu yanayovuka katika Mto Mara kila mwaka, na hivyo kuufanya kuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii nchini.


Makundi ya nyumbu yakivuka Mto Mara

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa Mto Mara unaanzia katika chemchem ya Enapuyapui kwenye misitu ya Milima Mau nchini Kenya na hutiririsha maji kupitia mbuga ya Masai- Mara (Kenya) na Hifadhi ya Taifa Serengeti kabla ya kumwaga maji yake ndani ya Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

Eneo la Bonde la Mto Mara lina ukubwa wa kilomita za mraba 13,325 huku mto huo ukiwa na urefu wa killomita 400.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages