NEWS

Sunday, 14 September 2025

Katibu Mkuu Mwajuma akagua Miradi ya Maji ya Miji 28 Mara



Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri (kulia mbele), akiongozwa na mkandarasi alipokwenda kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Tarime na Rorya, mkoani Mara jana.

Na Waandishi Wetu, Mara

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amekagua maendeleo ya utekelezaji wa Miradi ya Maji ya Miji 28 katika wilaya za Serengeti, Tarime na Rorya, mkoani Mara na kuwataka wakandarasi kuikamilisha kwa muda uliopangwa.

Akiwa wilayani Serengeti katika ziara hiyo ya kikazi aliyoifanya jana Jumamosi, Mhandisi Mwajuma alitembelea Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Mugumu unaotekelezwa katika eneo la Bwawa la Manchira, ambapo alijionea shughuli mbalimbali zinazoendelea na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi.

Alimwelekeza mkandarasi husika kuongeza nguvu kazi katika utekelezaji wa mradi huo ili ifikapo Desemba 2025 wananchi wa Serengeti waweze kupata maji ya uhakika.

Alisema azma ya serikali ni kutatua kero ya uhaba wa maji katika maeneo yote nchini, hivyo kukamilika kwa mradi huo kutaondoa changamoto ya maji kwa wakazi wa mji wa Serengeti.

"Kukamilika kwa mradi huu kutaondoa kabisa changamoto ya maji kwa wakazi wa mji wa Serengeti na maeneo ya jirani, hivyo hakikisheni unakamilika kwa wakati kwa kuongeza nguvu kazi na vifaa ili Desemba mwaka huu wananchi waanze kunufaika na maji ya uhakika," alisema Mhandisi Mwajuma.

Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Mugumu - Serengeti unaotekelezwa na Mkandarasi Mega Engineering and Infrastructure Company Limited kutoka nchini India kwa gharama ya shilingi bilioni 21.

Mradi huo unatarajia kukamilika Desemba 2025 ambapo kukamilika kwake kutasaidia kuondoa adha ya uhaba wa maji kwa wakazi zaidi ya 100,000 wa mji wa Serengeti na viunga vyake.


Katibu Mkuu Mhandisi Mwajuma Waziri akiongozwa na mkandarasi alipokwenda kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Mugumu katika eneo la Bwawa la Manchira, wilayani Serengeti jana.

Baada ya Serengeti, Katibu Mkuu Mhandisi Mwajuma alikwenda kukagua Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Tarime na Rorya, akianzia kituo cha usambazaji maji cha Mogabiri wilayani Tarime na kumalizia ukaguzi wake kwenye mtambo wa kuchuja maji Nyamagaro wilayani Rorya.

"Tumeridhika na kazi inayotekelezwa na mkandarasi, kama wizara tunasisitiza nguvu ya utekelezaji, msukumo mkubwa uendelee,” alisema Mhandisi Mwajuma na kuendelea:

"Hapa Tarime - Rorya tumeona wafanyakazi wapo wengi na kazi kubwa inafanyika, 'structures' 17 kati ya 20 zimekamilika… mkandarasi aongeze bidii ili ujenzi ukimbie kwa kasi.”

Mradi huo ambao utagharimu shilingi bilioni 134 kutoka serikalini, ukikamilika utawezesha maelfu ya wananchi wa Tarime na Rorya kuanza kutumia maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria.

Mhandisi Mwajuma aliendelea kusisitiza kuwa Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa nchini na imedhamiria kuhakikisha inamtua mama ndoo ya maji kichwani.

"Tumeona Tarime - Rorya serikali inatekeleza miradi ya kimkakati, wananchi watafurahi zaidi, wategemee mambo mazuri zaidi,” alisema.

Katika ziara hiyo ya kikazi, Katibu Mkuu Mhandisi Mwajuma aliambatana na viongozi watendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara na mamlaka za maji Mugumu, Tarime na Rorya.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages