
Nyumbu wakivuka Mto Mara
Na Mwandishi Wetu, Butiama
Maadhimisho ya 14 ya Siku ya Mto Mara yanafanyika leo Septemba 15, 2025 nchini Tanzania katika wilaya ya Butiama, mkoani Mara kwa ushirikiano na nchi ya Kenya.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu wa 2025 ni “Hifadhi Mto Mara. Linda Uhai”.
Wadau mbalimbali wa uhifadhi kutoka mataifa hayo mawili ya Afrika Mashariki wanashiriki katika maadhimisho hayo yanayotajwa kuwa na msukumo unaochangia uhifadhi endelevu wa Mto Mara.
Tanzania na Kenya zimekuwa zikiadhimisha Siku ya Mara Septemba 15 kila mwaka kwa kupokezana, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza juhudi za pamoja za uhifadhi endelevu wa Bonde la Mto Mara unaotiririsha maji katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania.
Kwa kutambua umuhimu wa ikolojia ya Mara, kikao cha 10 cha Sekretarieti ya Mawaziri wa Bonde la Ziwa Victoria kilichofanyika Kigali nchini Rwanda Mei 4, 2012 kiliazimia Septemba 15 kila mwaka kuwa Siku ya Mara.
Maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Mara yalifanyika mwaka 2012 nchini Kenya na kwa upande wa Tanzania maadhimisho ya kwanza ya siku hiyo yalifanyika mwaka 2013 katika mji wa Mugumu, wilayani Serengeti.
Mbali na umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori, inakadiriwa kuwa maisha ya watu zaidi ya milioni moja hutegemea uwepo wa Bonde la Mto Mara upande wa Tanzania na Kenya.
Aidha, watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani wamekuwa wakimiminika kushuhudia makundi ya nyumbu yanayovuka katika Mto Mara kila mwaka, na hivyo kuufanya kuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii nchini.
Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa Mto Mara unaanzia katika chemchem ya Enapuyapui kwenye misitu ya Milima Mau nchini Kenya na hutiririsha maji kupitia mbuga ya Masai- Mara (Kenya) na Hifadhi ya Taifa Serengeti kabla ya kumwaga maji yake ndani ya Ziwa Victoria upande wa Tanzania.
Eneo la Bonde la Mto Mara lina ukubwa wa kilomita za mraba 13,325 huku mto huo ukiwa na urefu wa killomita 400.
No comments:
Post a Comment