NEWS

Saturday, 13 September 2025

Serikali yataja matishio ya mazingira Mto Mara



Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, akizungumza kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Mto Mara mwilayani Butiama jana.


Na Mwandishi Wetu, Butiama

Serikali imesema juhudi za makusudi lazima zichukuliwe ili kutatua changamoto zinazoukabili Mto Mara mkoani Mara - ambao ni muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe wengine wanaoishi kando kando yake.

Mto Mara, ambao unatiririka kutoka Milima ya Mau nchini Kenya kupitia Hifadhi za Masai-Mara na Serengeti na kumwaga maji yake Ziwa Victoria, unakabiliwa na uharibifu wa misitu kando kando yake, uchimbaji madini usiozingatia sheria na uchafuzi wa maji kutokana na shughuli nyingine za binadamu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, akizungumza kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Mto Mara mwilayani Butiama jana, aliwataka wananchi, asasi za kiraia na wadau wa kimataifa kuhakikisha mazingira ya mto huo yanalindwa.

Maadhimisho ya Siku ya Mto Mara kwa mwaka huu yaliyobeba kaulimbiu inayosema “Hifadhi Mto Mara, Linda Uhai”, ambayo hufanyika Septemba 15 kila mwaka, ni fursa muhimu ya kutafakari umuhimu wa mto huo kwa nchi jirani za Tanzania na Kenya.

Katibu Mkuu Mwajuma aliwambia wananchi mjini Butiama kwamba uharibifu wa Mto Mara ni sawa na “kujiangamiza” kwa sababu ni chanzo cha maisha ya maelfu ya watu na viumbe hai wengine. “Kuhifadhi Mto Mara ni kuhifadhi maisha ya sasa na ya baadaye,” alisema.

“Tuimarishe elimu ya uhifadhi kwa wanafunzi shuleni, tuhimize matumizi endelevu ya ardhi, tushirikiane kudhibiti uvuvi haramu, uchafuzi wa maji, na tuwe mstari wa mbele kuripoti matukio ya uharibifu wa mazingira,” aliongeza.

Tanzania ni moja ya nchi zilizojaaliwa barani Afrika kuwa na vyanzo vingi vya maji kuanzia mito na maziwa makubwa kama vile Victoria, Tanganyika na Nyasa, achilia mbali maziwa madogo ya ndani.

Katika miongo ya hivi karibuni, serikali imekuwa ikijitahidi kubuni sera za kulinda vyanzo hivyo vya maji katika dunia ambayo wataalamu wa mazingira na haidrolojia wanaonya kwamba huenda miongo michache ijayo ikakabiliwa na janga la uhaba wa maji na vita ya kugombania rasilimali hiyo.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages