NEWS

Monday, 20 October 2025

Benki ya CRDB yawazawadia wanafunzi watatu bora Sekondari ya Magrethmary



Mwakilishi wa mgeni rasmi akikabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa kidato cha nne wakati wa Mahafali ya Kwanza ya Shule ya Sekondari Magrethmary, Oktoba 17, 2025.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
-------------

Benki ya CRDB Tawi la Sirari imewapa wanafunzi bora watatu wa Shule ya Sekondari Magrethmary iliyopo kata ya Regicheri, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), zawadi ya kuwafungulia akaunti na kuwawekea fedha katika benki hiyo.

Benki hiyo ilikabidhi zawadi hiyo wakati wa Mahafali ya Kwanza ya Wahitimu 21 (wasichana 11 na wavulana 10) wa Kidato cha Nne yaliyofanyika shuleni hapo Oktoba 17, 2025.


Wahitimu wa kidato cha nne wakiimba na kucheza kwa madaha wakati wa mahafali yao

Aidha, mgeni rasmi ambaye aliwakilishwa na Mdhibithi Ubora wa Huduma wa benki hiyo, Ramadhani Allay, pia aliahidi kuipatia kompyuta mbili ili kuinua kiwango cha taaluma.

Alitumia nafasi hiyo pia kueleza kuwa benki hiyo inaanzisha mpango maalum wa 'Ada Loan' utakaowezesha wazazi kulipiwa ada za watoto wao kisha kurejesha kidogo kidogo bila kwenda benki.


Mwakilishi wa mgeni rasmi akikabidhi cheti kwa mhitimu

"CRDB tupo tupo hatua za mwisho kukamilisha mpango wa 'Ada Loan', tukifanya makubaliano na Mkurugenzi wa Shule, mzazi anaweza akalipiwa ada na benki halafu akarudisha taratibu taratibu, haihitaji kuja benki wala kujaza fomu - inafanyika kwa njia ya simu,” alisema.

Awali, Mwalimu wa Taaluma wa Sekondari ya Magrethmary, Chacha Marwa, alisema shule hiyo ilishika nafasi ya kwanza kiwilaya na ya nne kimkoa katika mtihani wa upimaji kidato cha pili wanafunzi mwaka huu.


Mwakilishi wa mgeni rasmi na walimu wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa Mahafali ya Kwanza ya Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Magrethmary. (Picha zote na Mara Online News)

"Aidha, katika mtihani Kanda ya Ziwa mwaka huu, karibu wanafunzi wote wa kidato cha nne walifaulu kwa kupata daraja la kwanza, huku mmoja akipata daraja la tatu, shule ikawa ya nne kiwilaya kati ya 45, ya 12 kimkoa kati ya 260 na ya 91 kikanda kati shule 1,401,” alisema mwalimu Marwa na kuongeza:

"Mwaka 2025, kwenye utahini kidato cha nne shule yetu iliongoza kwa kushika nafasi ya kwanza kiwilaya kati ya 41, ambapo pia masomo saba kati ya 10 tuliongoza kwa kushika nafasi ya kwanza kiwilaya kwa masomo ya Uraia, Historia, Kiswahili, Kiingereza, Baiolojia, Hesabu na Fasihi ya Kiingereza.”

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages