
Balozi wa Poland nchini Tanzania, Sergiusz Wolski na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly, wakiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali na watoto ambao ni wanufaika, wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi wa majengo mapya ya Butiama Nyumba Salama inayoendeshwa na shirika hilo, jana Jumapili.
Na Mwandishi Wetu
Butiama
--------------
Balozi wa Poland nchini Tanzania, Sergiusz Wolski, amezindua rasmi mradi wa majengo mapya ya Butiama Nyumba Salama inayoendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT).
Majengo hayo yatatumika kulinda wasichana dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuwawezesha kufikia ndoto zao za kielimu, kwa mjibu wa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Rhobi Samwelly.
Ufunguzi huo ulifanyika jana Jumapili ambapo ulihudhuriwa na wageni mbalimbali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Thecla George Mkuchuka.

Balozi wa Poland nchini Tanzania, Sergiusz Wolski (katikati), akikata utepe kufungua rasmi majengo mapya ya Nyumba Salama Butiama iliyopo chini ya Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, mkoani Mara jana Jumapili.
“Nimefurahi sana kuwa mmekuja kuungana nasi kusherehekea uzinduzi wa majengo, na kikubwa ni kulinda wasichana na wanawake na kuimarisha maisha yoa,” Rhobi ambaye pia ni mwanzilishi wa Shirika hilo la HGWT alieleza katika hafla hiyo.
Risala ya watoto ambao ni wanafuka ilisema mradi huo umehusisha majengo ya utawala na samani zake, bwalo la chakula na jiko lake, mabweni mawili - kila moja likiwa na vyumba 20 vyenye uwezo wa kuchukua vitanda 80, vyumba viwili vya madarasa, karakana, uwanja mpira wa kikapu, vifaa vya michezo na uzio.
Mradi huo wa majengo umefadhiliwa na Serikali ya Poland kupitia shirika lake la Polish Aid kwa kushirikiana na Taasisi ya Kiabakari.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu Rhobi, hadi sasa shirika la HGWT limeshatoa hifadhi salama kwa wasichana 3,277 waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni na kuwasaidia wasichana 1,232 kurejea shuleni na kuendelea na masomo yao.
Pia, shirika hilo limeweza kutoa mafunzo ya ujuzi wa maisha (life skills) kwa wasichana 3,262 ndani ya Nyumba Salama na kufanikisha kampeni ya uelimishaji jamii ambapo watu zaidi ya 100,000 wamefikiwa kupitia mikutano, redio na shule.
Aidha, HGWT imeanzisha na kuendeleza mradi wa ushonaji wa sweta unaofanyika katika Nyumba Salama Butiama.
Kwa upande wake Balozi Wolski alipongeza wadau wote walioshiriki kutekeleza katika mradi huo kwa mafanikio makubwa.
Alisema suala la ukatili ya kijinsia ni tatizo lililopo maeneo mbalimbaIi na hivyo kuhimiza juhudi za pamoja katika kulitokomeza.
Balozi huyo alifurahi pia kuona uwepo wa wadau muhimu kama Jeshi la Polisi, mahakama na viongozi wa dini katika hafla hiyo.

Kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Thecla George Mkuchuka, Mkurugenzi wa HGWT, Rhobi Samwelly na Balozi Wolski wakikagua majengo hayo. (Picha zote na Mara Online News)
Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania limekuwa mstari wa mbele katika kupiga vita vitendo vya ukaitli wa kinjisia ambayo pamoja na mambo mengine vimekuwa vikichangia kukatisha ndoto za elimu kwa wasichana katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mara.
Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa shirika hilo limeokoa mamia ya wasichana waliokuwa katika hatari ya kukeketwa na kuwasaidia baadhi yao kufikia ndoto zao za kielimu.
Mara ni moja ya mikoa inayoripotiwa kuwa na vitendo vingi vya ukatilii wa kijinisia, huku taarifa za serikali zikionesha takwimu za matuko hayo zinaendelea kupungua, shukrani kwa wadau wote wanaosaidia kampeni ya kupinga ukatili wa kijinisia katika mkoa huo.
No comments:
Post a Comment