
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (katikati waliokaa), Mkurugenzi Mtendaji wa Professor Mwera Foundation (PMF), Hezbon Peter Mwera (kushoto), Mwakilishi wa Soya One Limited, Mwita Meck na Mkuu wa Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko, Mwalimu Mwita Samson Marwa (kushoto waliosimama), wakiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa kidato cha nne shuleni hapo Oktoba 17, 2025.
Na Mwandishi Wetu
Tarime
------------
Tarime
------------
Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko imesherehekea Mahafali ya Nane Kidato cha Nne 2025 huku mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akiipongeza kwa maendeleo ya kitaaluma yanayoiwezesha kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.
Mahafali hayo yalifanyika Oktoba 17, 2025 katika shule hiyo inayomilikiwa na Taasisi ya Professor Mwera (PMF), nje kidogo ya mji wa Tarime, mkoani Mara.

Wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko wakiwa katika mahafali yao.
"Kipekee niwapongeze sana kwa matokeo mazuri, nimeona mmefuta zero (sifuri) na mmekuwa mfano kwa shule za Tarime kwa kuonesha kwamba inawezekana kukiwa na mikakati mizuri," Meja Gowele alisema katika hotuba yake.

DC Gowele akikabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko wakati wa mahafali hayo.

DC Gowele akiendelea kukabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko wakati wa mahafali hayo.
Kwa mujibu wa Mwalimu wa Taaluma wa sekondari hiyo, Mohagachi Matiko, wanafunzi wanaohitimu ni 36 (wasichana 23, wavulana 13), ambao walianza kidato cha kwanza mwaka 2022, na kwamba ufaulu ulisababisha wengine 10 kujiunga na shule hiyo.
"Hawa wanaohitimu leo walianza kidato cha Kwanza mwaka 2022 na walikuwa 23 tu, lakini kwa sababu ufaulu wa shule yetu ni mkubwa wanafunzi wengi wanapendelea kuja hapa na hata wazazi pia wanavutiwa na shule yetu," alisema Mwalimu Mohagachi.

DC Gowele akkabidhi cheti kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya PMF, Hezbon Peter Mwera.

DC Gowele akkabidhi cheti kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko, Mwalimu Mwita Samson Marwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya PMF), Hezbon Peter Mwera, alisema shule hiyo ni miongoni mwa sekondari zilizoruhusiwa kutoa elimu ya ufundi "mkondo wa amali" kwa wanafunzi wake.
"Sisi kama taasisi tumekuwa moja ya wadau walioshawishi sana wizara kuanzisha mkondo wa amali, na shule yetu ya Tarime Mchanganyiko ni moja ya sekondari zilizopewa mkondo wa amali - kwa maana kwamba, mbali na masomo ya kawaida, pia mtoto anasoma fani moja ya ufundi," alisema Hezbon.

DC Gowele akikabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko wakati wa mahafali hayo.
Viongozi wengine walioalikwa kwenye mahafali hayo ni pamoja na mwakilishi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Soya One Limited aliyeichangia shule hiyo shilingi 1,000,000 na mgombea ubunge katika jimbo la Tarime Mjini, Esther Matiko, aliyechangia shilingi 500,000 kwa ajili ya ununuzi wa chanzo cha umeme wa ziada.
Mbali na Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko, Taasisi ya PMF inamiliki pia Shule ya Msingi Mwera Vision, Jogging Club, Mwera Jazz Band, PMF Restaurant na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime kinachotoa mafunzo ya fani tofauti zikiwemo za ufundi magari, umeme, mabomba, uhazili, udereva, ushonaji, uongozaji watalii na upishi, miongoni mwa nyingine.
No comments:
Post a Comment