NEWS

Saturday, 25 October 2025

DC Gowele awapongeza wanahabari Tarime akizindua umoja wao



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kushoto), akimkabidhi Mwenyekiti wa Umoja wa Kuwezesha Waandishi wa Habari (REU), Jacob Karoli mchango wa kutunisha mfuko wa umoja huo katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika kwenye ukumbi wa CMG Hotels jana Oktoba 24, 2025.

Na Christopher Gamaina
Tarime
-----------

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele, amewapongeza waandishi wa habari wa wilayani humo kwa mchango wao mkubwa katika kuhabarisha jamii na kuibua changamoto zinazokabili wananchi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuandika habari kwa weledi na uzalendo ili kulinda amani na mshikamano wa eneo hilo.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Umoja wa Kuwezesha Waandishi wa Habari (REU) Tarime, kwenye ukumbi wa CMG Hotels jana usiku, Meja Gowele alisema wanahabari ni nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii.

Kwamba kupitia kalamu zao, serikali inapata mrejesho wa changamoto na mafanikio yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali.

“Waandishi wa habari ni mkono wa serikali. Kama mkuu wa serikali kwenye wilaya mmekuwa mkinipa ushirikiano mkubwa, na wakati mwingine mmekuwa mkiibua changamoto zilizopo kwenye jamii, inatusaidia kutoka kwenda kuzishughulikia,” alisema.
Akizungumzia REU, Meja Gowele aliwapongeza wanahabari hao kwa kuona umuhimu wa kuanzisha umoja huo, akiutaja kama chombo muhimu kitakachowezesha kurekebishana na kuboresha maisha yao.

“Niwapongeze waandishi wa habari kwa maamuzi yenu ya kujiunga ili muwe kitu kimoja - kama platform nzuri ya ninyi kushauriana, lakini pia kuimarisha maisha yenu na kazi zenu, hongereni sana,” alisema na kuendelea:.

“Naamini umoja huu utakuwa platform nzuri ya ninyi kujadiliana na kushauriana namna ya kufanya kazi na jamii zetu, wawekezaji, taasisi za umma na binafsi. Tunaamini mtakuwa mnajifunza kwa kuelezana ‘hapa mwenzetu uliteleza – rekebisha’.

“Mkiandika jambo litakaloleta taharuki mnaweza mkawa chanzo cha matatizo katika wilaya yetu. Tujikite zaidi kwenye kutangaza mazuri yaliyopo Tarime, tunayo mazuri mengi sana ya kuandika.”
Mgeni Rasmi, DC Meja Gowele alikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa REU.

Meja Gowele aliwakumbusha wanahabari kuwa uhuru wa vyombo vya habari una mipaka na kwamba kalamu zao zinapaswa kuwa chombo cha kujenga, si kubomoa. “Usiandike stori kwa ajili ya kumwangamiza mtu, andika kwa manufaa ya jamii,” alisema.

“Mkifanya balancing kwenye stories zenu hamtaingia migogoro na watu - hamtaingia migogoro na wawekezaji, hamtaingia migogoro na serikali. Uhuru wa vyombo vya habari ni mkubwa lakini lazima tutambue una mipaka,” alisisitiza Meja Gowele.

Pia, aliwashauri kujenga uhusiano na wadau wa maendeleo, wakiwemo wawekezaji, taasisi za umma na binafsi, akitaja mifano ya taasisi zinazochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa Tarime kama Chichake Sports Bar and Grill, Soya One Limited, CMG Hotels, WAMACU Ltd, Alkos Elution Plant na benki, zikiwemo, CRDB, NBC na NMB.

Aligusia sekta ya kilimo akisema Tarime imebarikiwa kuwa na misimu miwili ya mvua kwa mwaka na kwamba juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, zilizowezesha ujenzi wa soko la kisasa la mazao eneo la Regicheri, ni kielelezo cha dhamira ya serikali katika kuboresha maisha ya wananchi.

Kuhusu vivutio vya utalii, alisema wilaya ya Tarime inabeba sehemu kubwa ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, likiwemo eneo maarufu la Kogatende ambako makundi ya nyumbu huvuka Mto Mara kwenda nchi ya Kenya na Kurudi Tanzania kila mwaka.

Meja Gowele alisema eneo hilo linastahili kutangazwa zaidi ili kuongeza idadi ya watalii na kukuza uchumi wa Tarime.

“Maajabu ya dunia yako pale [Kogatende]. Tutumie kalamu zetu kutangaza mazuri hayo, ni kivutio kikubwa kwenye wilaya yetu. Lakini pia kuna wawekezaji wakubwa wako pale. Kwa hiyo, mzunguko mkubwa wa fedha uko katika wilaya yetu,” alisema.

Aliwapongeza wadau mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa REU na kutoa michango ya fedha kwa ajili ya kutunisha mfuko wa umoja huo.

“Niwapongeze wadau wote mlioitika kuja kuwashika mkono ndugu zetu waandishi wa habari. Wananchi wanategemea kalamu zao kuweza kujua dunia inavyokwenda. Hivyo, wawe sehemu ya kuandika vitu ambavyo vitalinda uhuru wetu, utamaduni wetu na maadili yetu,” alisema.

Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza pia umuhimu wa waandishi wa habari kujiendeleza kitaaluma ili kuongeza weledi wao katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Elimu haina mwisho, mimi mpaka sasa ninasoma. Kwa hiyo, hata ninyi kwenye tasnia yenu mjiendeleze ili mfanye vizuri zaidi,” alisema Meja Gowele.

Aliwahakikishia waandishi wa habari kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao kwa karibu katika kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa uhuru, lakini ndani ya mipaka ya kisheria na maadili ya taaluma.

“Mimi kama mkuu wa serikali kwenye wilaya nitahakikisha taasisi zote za umma zinawapa ushirikiano pale mtakapohitaji, na mkikwama basi tuwasiliane, kama ni taarifa ambayo hairuhusiwi utaambiwa,” alisema.
Meja Gowele alihitimisha hotuba yake kwa kutoa wito wa kuwataka wananchi kuepuka uchochezi na uzushi kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, akisema serikali imejipanga kuhakikisha unafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na usalama.

“Tunawatahadhirisha wananchi kuepuka uchochezi na uzushi, ikiwemo kupitia mitandao ya kijamii. Watu wajitokeze kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi. Niwahakikishie tutafanya uchaguzi katika mazingira ya amani na utulivu kwani serikali tumejipanga vizuri,” alieleza.

Awali, wadau waliohudhuria uzinduzi wa REU, wakiwemo Mkurugenzi wa Chichake Sports Bar and Grill, Nicolaus Mgaya Chichake, wawakilishi wa Soya One Limited na WAMAVU Ltd waliahidi kuendelea kushirikiana na wanahabari katika kujenga wilaya ya Tarime kijamii na kiuchumi.

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa Meja Gowele na Mwenyekiti wa REU, Jacob Karoli, kuongoza harambee ndogo ya umoja huo iliyofanikisha upatikanaji wa shilingi milioni 11, ambapo DC huyo alitoa shilingi 650,000 zikiwemo za kusindikizwa na rafiki zake.

Wengine waliochangia ni pamoja na Chichake aliyetoa shilingi milioni 1.5, Soya One Limited (shilingi milioni moja) na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye “Namba Tatu” (shilingi milioni moja), miongoni mwa wadau wengine.

Mkurugenzi wa Chichake Sports Bar and Grill, Nicolaus Mgaya Chichake, akizungumza katika hafla hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages