
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas (aliyevaa suti), akizindua Programu Tumizi ya TANAPA GO katika hafla iliyofanyika kwenye Hifadhi ya Taifa Mikumi jana. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara na wa nne kulia ni Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Masana Mwishawa.
Na Mwandishi Wetu
Morogoro
---------------
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) jana Alhamisi lilizindua Programu Tumizi ya TANAPA GO kuwa daraja la kukuza na kuongeza maendeleo ya sekta za uhifadhi na utalii nchini
Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Masana Mwishawa, App hiyo inatarajiwa kuchangia kwa upana upatikanaji wa taarifa za hifadhi kwa wepesi kwa watalii wanaotembelea au wanaopanga kutembelea hifadhi za taifa.
Programu Tumizi hiyo ilizinduliwa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, katika Hifadhi ya Taifa Mikumi, mkoani Morogoro.
Dkt. Abbas aliipongeza TANAPA kwa kutangaza shughuli za utalii kupitia teknolojia ya simu janja akieleza kuwa watu bilioni 5.7 duniani kote ni watumiaji wa intaneti na hivyo Programu Tumizi hiyo itatatua “changamoto yetu kubwa ya kujitangaza katika soko la utalii duniani.”
“Programu Tumizi hii itaturahisishia mambo mengi, itatusaidia kujua fursa za uwekezaji zinazopatikana katika hifadhi zote za taifa,”alisema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara, alisema programu hiyo itaongeza ufanisi katika shughuli za uhifadhi na utalii huku akiipongeza menejimenti ya TANAPA kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia.
“App hii ya TANAPA GO itaimarisha utendaji wa shirika kwa kuwa huduma na taarifa mbalimbali zitawafikia wageni ndani na nje ya nchi kwa haraka,” alieleza.
TANAPA ni moja ya mashirika makubwa yaliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo mchango wake mkubwa umeleta mapinduzi ya mapato kutokana na shughuli za utalii.
Ni moja ya mashirika yaliyoanzishwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere ili kuboresha maendeleo ya sekta ya utalii, ikizingatiwa kwamba Tanzania ni moja ya mataifa ya Afrika yenye hifadhi nyingi za taifa ambazo ni vivutio vikubwa kwa watalii duniani.
No comments:
Post a Comment