NEWS

Friday, 10 October 2025

Ujenzi mgodi wa madini ya kinywe wazinduliwa Morogoro




Na Mwandishi Wetu
Mahenge
---------------

Ujenzi wa mgodi wa madini ya kinywe ulizinduliwa rasmi jana huko wilayani Ulanga, Mahenge mkoani Morogoro, ikiwa ni hatua ya kutekeleza miradi ya kimkakati katika sekta ya madini nchini Tanzania.

Kinywe ni miongoni mwa madini muhimu kwa utengenezaji wa betri za magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki, paneli za umeme na umeme wa jua.

Kupitia miradi ya kinywe nchini, Tanzania inajiweka kuwa kitovu cha malighafi za teknolojia safi duniani.

Uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo, unaotekelezwa na Kampuni ya Faru Graphite Corporation kwa ubia na Serikali ya Tanzania na Black Rock Mining Limited, ulifanywa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

"Mradi huu si uchimbaji wa rasilimali pekee, bali ni injini ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa viwanda, biashara, ajira na ustawi wa jamii katika eneo la Mahenge kwa ujumla," alisema Mavunde.

Alisema mradi huo utagharimu dola za Marekani milioni 519 (zaidi ya Tsh trilioni 1.3) na unatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 400 wakati wa ujenzi na zaidi ya 900 za kudumu mgodi utakapoanza uzalishaji.

Pia mgodi huo utachochea ajira zaidi ya 4,500 kupitia mnyororo wa thamani.

Moja ya mambo ya msingi yatakayozingatiwa na wamiliki wa mgodi huo ni ushirikishwaji wa Watanzania na uwajibikaji kwa jamii kwa kutoa kipaumbele cha ajira kwa wanavijiji jirani na kampuni za ndani kushiriki katika mnyoroto wa ugavi.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, alisema mkoa wake umebahatika kuwa na miradi mikubwa ya maendeleo na akawataka wataalamu kuwaelimisha wananchi kuhusu fursa za kiuchumi na kijamii za mradi huo wa kinywe.

Naye Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, alisema wananchi 254 tayari wamelipwa fidia kupisha mradi huo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages