NEWS

Wednesday, 8 October 2025

Mugumu: Wataalamu wazuru eneo lililotengwa kujengwa Uwanja wa Ndege Serengeti




Na Mwandishi Wetu
Serengeti
---------------

Wataalamu kutoka Taasisi za Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Wahadhiri wa Uchumi - Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jana Oktoba 7, 2025 walikutana na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kujadili na kupata uelewa wa pamoja kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege wilayani Serengeti.

Aidha, baada ya mjadala kati ya taasisi hizo na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, timu hiyo ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Dkt. Maulid Suleimani Madeni, ilitembelea na kukagua eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi huo katika kata ya Uwanja wa Ndege, nje kidogo ya mji wa Mugumu.

Mwanzoni mwa mwaka huu, TAA ilitiliana saini na Kampuni ya Saba Engineering mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti katika halmashauri hiyo.

Ujenzi wa Uwanja wa Ndege Serengeti mkoani Mara ambao kwa miaka 20 umekuwa ukisuasua sasa umepata msukumo mpya baada ya utekelezaji wake kuingizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2025-2030.

Ilani hiyo mpya ya CCM ilizinduliwa rasmi Mei 30, 2025 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa sasa anatetea Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Ilani hiyo ya CCM, uwanja huo ni moja ya miradi kadhaa ya viwanja vya ndege nchini iliyopangwa kutekelezwa ndani ya miaka mitano ijayo ili kuimarisha sekta ya usafiri wa anga.

Lengo kubwa la ujenzi wa Uwanja wa Ndege Serengeti ni kuifungua na kuifanya wilaya hiyo kuwa kitovu cha utalii, ikizingatiwa kuwa eneo lake kubwa ni hifadhi kongwe na bora Afrika – Hifadhi ya Taifa Serengeti ambayo ni kivutio kikubwa cha watalii duniani.

Ujenzi wa uwanja huo utawezesha watalii kutoka nje kutua moja kwa moja katika mji wa Mugumu ambao mamlaka zimekuwa zikijadiliana kubadili jina lake liwe Serengeti.

Pia, kujengwa kwa uwanja huo kutasaidia kupunguza idadi ya ndege zinazotua ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na kusaidia kufungua fursa za kiuchumi wilayani Serengeti, mkoa wa Mara na taifa kwa ujumla.

Katika miaka ya hivi karibuni, sekta ya usafiri wa anga nchini imeshika kasi kufuatia ujenzi wa barabara, reli ya kisasa, viwanja vya ndege na kuboreshwa kwa usafiri wa majini katika maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Uimarishwaji wa viwanja vya ndege umewavuta watalii wengi kutembelea maeneo mbalimbali ya Tanzania na kuliwezesha taifa kukusanya fedha nyingi za kigeni.

Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025-2030 pia imejumuisha ujenzi wa barabara ya lami ya Tarime hadi Mugumu, ikiwa ni jitihada za kuunganisha wilaya mbili za Tarime na Serengeti kwa miundombinu hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages